Upo Hapa: Home

ADHABU YA KIFO NI HALALI KWA MUJIBU WA SHERIA- PROF MCHOME

E-mail Print PDF

 

Adhabu ya kifo ni adhabu halali kwa mujibu wa sheria za nchi na inaweza kutolewa kwa wahalifu watakaotiwa hatiani kwa kutenda kosa husika na utekelezaji wake unabaki mikononi mwa mamlaka husika.

“Adhabu hiyo ni adhabu halali, inaweza kutolewa kwa yeyote atakaebainika kutenda makosa yanayostahiki adhabu hiyo na ndio maana bado ipo katika vitabu vyetu vya sheria, kwani sababu zilizopelekea kuwekwa kwa adhabu hiyo bado zipo,”  Prof Mchome.

Prof Sifuni Mchome Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria aliyasema hayo jijini Dar es Salaam kupitia kipindi Maalum cha TV cha TUNATEKELEZA kilichorushwa na Televisheni ya Taifa TBC1 juzi usiku kufuatia swali aliloulizwa na mwendesha kipindi kwamba haoni adhabu hiyo kama inapaswa kuacha kutumika nchini.

Alisema Serikali ilifanya utafiti na kugundua kuwa wananchi wengi bado wana imani na uwepo wa adhabu hiyo kwani wanasema adhabu hiyo ipo na hali ya makosa ya ajabu bado ipo itakuwaje adhabu hiyo ikiondolewa? Na kuongeza kuwa kuna hisia kuwa adhabu hiyo ikiondolewa na hali halisi ya kitanzania watu watakuwa hawana namna ya kuacha vitendo hivyo kwani hawatakuwa na cha kuogopa na vitendo hivyo vitaongezeka nchini.

“Tumefanya utafiti na kubaini kuwa adhabu hii inastahili kuendelea kutumika nchini , inaaminika kuwa itasaidia kupunguza vitendo vya kihalifu nchini, nchi yetu bado changa na ina safari ndefu kufikia maendeleo,  mtu anawezxa kuwa na chuki tu na mwingine na kumfanyia kitu kibaya , adhabu hii itasaidia kupunguza msukumo wa watu kutokufanya vitendo vya kihalifu ambavyo vitawafanya wastahili adhabu husika, vinginevyo watu hawatajali kwani hawatakuwa na cha kupoteza,” alisema Prof Mchome.

Alisema kuwa adhabu huwekwa katika vitabu vya sheria kwa sababu maalum sio kwamba zinatungwa tu ili mradi na kufafanua kuwa sababu zilizopelekea kutungwa kwa adhabu hii bado zipo hadi hii leo tunazo .

Alikiri kwamba Adhabu ya kifo ni suala la mjadala wa kimataifa kutokana na kwamba linamnyang’anya mwanadamu haki yake ya kuishi lakini kwa nchi yetu bado serikali inaamini kuendelea kuitumia adhabu hii.

Aliongeza kuwa kama utafika wakati ambapo tutaona kuwa ni uafaka kuiondoa hii adhabu basi tutafanya hivyo na tutakuwa tumejihakikishia kuwa vitendo hivyo vilivyosababisha kuwepo kwake vimeondoka na kuisha kabisa au kupungua na pia kuangalia kama adhabu mbadala itakidhi lengo la adhabu hiyo iliyowekwa awali kufikiwa

Sheria lazima ziogopwe, zisipoogopwa nguvu ya sheria haitakuwepo, sheria hutungwa ili kuwazuia watu kufanya vitendo ambavyo vitawapelekea kufikishwa katika mikono ya sheria na kupelekwa katika mahakama. Lengo la serikali ni kuhakikisha rasilimali za taifa zilizopo zinaenda katika miradi ya maendeleo na sio kuishia kutoa huduma katika magereza. Wananchi wana wajibu wa kuhakikisha wanazingatia sheria na kuzitii bila ya shuruti.

-Mwisho-

 

Matukio Mapya

Hakuna Tukio kwa sasa.

Anuani

KATIBU MKUU

  • Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria,
  • Barabara ya Mkalama,
  • Jengo la Taaluma Na. 1,
  • Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria cha Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM,
  • S.L.B. 315,
  • DODOMA.
  • Simu:+255 26 2321680
  • Nukushi: +255 26 2321679
  • Tovuti www.sheria.go.tz
  • Barua pepe: km@sheria.go.tz