Upo Hapa: Habari
Habari | Wizara ya Katiba na Sheria
E-mail Print PDF

Habari mpya - Habari mpya
SHERIA ZOTE KUPATIKANA MTANDAONI
Administrator - Monday, 17 July 2017

SHERIA ZOTE KUPATIKANA MTANDAONI

Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi asema Wizara ya Katiba na Sheria itahakikisha sheria zote zitapatikana kwenye mtandao.

“Wizara itahakikisha sheria zote zitapatikana kwenye mtandao” Prof. Kabudi alitoa ahadi hiyo alipotembelea Mahakama ya Tanzania leo (14/7/2017) jijini Dar Es Salaam baada ya kupata taarifa juu ya utendaji kazi wa Mahakama nchini kote.

Waziri Kabudi amesema kwa kushirikiana na Mahakama na wadau wengine Wizara itahakikisha inarahisisha upatikanaji wa sheria zote kwa wananchi kwa kuziweka mtandaoni ili wananchi wanapozihitaji waweze kuzipata kwa urahisi mtandaoni bila kwenda kuziomba Wizarani, Mahakama au Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Waziri Kabudi amesema kati ya mihimili ya nchi Mahakama ndio mlinzi mkuu wa Katiba ya nchi hivyo ina haja ya kulinda uhuru wa Mahakama na kutenda haki kwa wananchi wote na vilevile kuondo taswira hasi kwa jamii juu yao na kuongeza ushirikiano na jamii.

Awali akimkaribisha Waziri Kabudi, Kaimu Jaji Mkuu wa Mahakama  Mhe. Prof. Ibrahim Juma alisema wananchi wanamtegemea sana Waziri wa Katiba na Sheria kustawisha na kubadilisha maisha yao kwa kupitia sheria za Tanzania, hivyo Sheria zitakazokuwa zikitungwa zitatoa nafuu kwa wananchi na kupunguza mlolongo wa kesi Mahakamani ili kuwapa fursa wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Kwa sasa Mahakama ya Tanzania kupitia namba ya simu waliyotoa kwa wananchi wamekuwa wakipokea malalamiko machache ya vitendo vya rushwa na kadhia nyingine walizokuwa wanakutana nazo wanapofatilia kesi zao Mahakamani na hivyo kupata muda zaidi wa kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Habari mpya - Habari mpya
WIZARA YAWASILISHA MPANGO NA MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA KWENYE KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2017/2018
Administrator - Monday, 03 April 2017

WIZARA YAWASILISHA MPANGO NA MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA KWENYE KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2017/2018

Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria imewasilisha Mpango na Makadirio ya Bajeti yake na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge mjini Dodoma.

Taarifa hiyo imewasilishwa na Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Mhe. Prof Palamagamba Kabudi mjini Dodoma na kuhudhuriwa na watendaji mbalimbali wa Wizara wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bw. Amon Mpanju, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Mdemu, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora mhe. Thom Bahame Nyanduga na viongozi na watendaji wa Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara.
Wizara pia iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2016/17.
Akiwasilisha taarifa hiyo Mhe. Prof Palamagamba Kabudi amesema katika mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara itaendeleza juhudi za kuimarisha utawala wa sheria na misingi ya haki za binadamu nchini kwa kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma bora na za uhakika.
Mhe. Prof Kabudi alitaja vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2017/18 kuwa ni kuendelea na uhamishaji wa shughuli za Serikali kutoka Dar es Salama kuja makao makuu ya nchi, Dodoma; Kuimarisha mfumo wa sheria na kuongeza uwezo wa Wizara katika maeneo maalum ya sheria, usimamizi na utoaji haki; Kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa masuala ya Katiba na sheria; Kuimarisha misingi ya haki za binadamu na kisheria; Kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika shughuli za utawala na uendeshaji; Kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mpango wa maboresho ya mahakama nchini; na Kuwajengea uwezo watumishi ili kuendeleza ubunifu na weledi ili kuleta tija na ufanisi.

Wizara ya Mambo ya Katiba inazo taasisi Tisa inazozisimamia ambazo ni Mahakama ya Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Wakala wa usajili, Ufilisi na Udhamini -RITA, Chuo cha Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo, chuo cha Uongozi wa Mahakama na Tume ya Kurekebisha Sheria.

Habari mpya - Habari mpya
DKT. MWAKYEMBE AKABIDHI OFISI KWA PROF. KABUDI
Administrator - Thursday, 30 March 2017

DKT. MWAKYEMBE AKABIDHI OFISI KWA PROF. KABUDI

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amekabidhi Ofisi rasmi kwa Waziri mpya wa Katiba na Sheria Prof Palamagamba Kabudi makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Dkt. Mwakyembe ambaye ni  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ameahidi kumpa ushirikiano Waziri mpya wa Katiba na Sheria kwa kuwa wizara hii ni nyumbani  kwake na kuwaasa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa moyo mmoja na kumpa ushirikiano unaotakiwa Waziri mpya ili kuhakikisha gurudumu la Sekta ya Sheria linasonga mbele

Naye Waziri wa Katiba na Sheria Prof Palamagamba Kabudi ameahidi kuyaendeleza yale yote ambayo Dkt Mwakyembe aliyaanzisha ili kuhakikisha yanakamlika na kutumiza ndoto zake. Amesema alivyoteuliwa kuongoza Wizara hiyo sio kwamba anakuja na vitu vyake vipya ila ataendeleza yake yote ambayo mtangulizi wake aliyafanya.

"Sikuja kutengua Torati, nimekuja kuikamilisha" alisema Prof Kabudi.

Alimueleza Dkt Mwakyembe kwamba yeye na Wizara yake wataendelea kuyahitaji mawazo yake na hivyo siku ikitokea hivyo hatosita kumfuata. “Kuondoka kwako katika wizara hii sio kwamba ndio mwisho, wewe ni mwenzetu, tuna imani  kwamba huku ni nyumbani kwako, usituache na kututupa , tutaendelea kufuata hekima na ushauri wako ili tuiendeleze sekta ya sheria nchini kwa pamoja”, alisema Prof Kabudi.

Aliwataka watumishi wa wizara kuendelea kuchapa kazi bila ya kujali kazi gani mtu anafanya kwakuwa kazi zote ni sawa na hatobagua mtu kwa kwa kazi yake kwakuwa kila mtu ana umuhimu wake wizarani.

 

Habari mpya - Habari mpya
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA PROF PALAMAGAMBA KABUDI AWASILI OFISINI MJINI DODOMA
Administrator - Tuesday, 28 March 2017

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA PROF PALAMAGAMBA KABUDI AWASILI OFISINI MJINI DODOMA

Waziri wa Katiba na Sheria Prof.Palamagamba Kabudi amewasili katika Ofisi za Makao makuu ya Wizara zilizoko ndani ya Chuo Kikuu cha Dodoma na kulakiwa na watumishi wa Wizara walioko makao makuu ya Serikali mjini Dodoma. Prof Kabudi aliapishwa tarehe 24/03/2017 Ikulu jijini Dar Es Salaam kuchukua nafasi hiyo baada ya Mhe.Rais kufanya mabadiliko madogo kwenye Baraza la Mawaaziri ambapo Dkt. Harrison Mwakyembe alihamishiwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Nje ya Ofisi za Wizara Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi alilakiwa na Naibu Katibu Mkuu, Bw. Amon Mpanju, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Aloyce Mwogofi, Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma na wafanyakazi wengine wa Wizara waliopo Makao Makuu ya Serikali mjini Dodoma.

Habari mpya - Habari mpya
DKT. MWAKYEMBE AZINDUA RASMI OFISI ZA WIZARA YAKE MKOANI DODOMA
Administrator - Thursday, 02 February 2017

DKT. MWAKYEMBE AZINDUA RASMI OFISI ZA WIZARA YAKE MKOANI DODOMA

DODOMA.

Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amezindua rasmi Ofisi za wizara yake mkoani Dodoma na kuwataka Watumishi wa wizara waliohamia Makao Makuu ya Serikali, Dodoma kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Dkt Mwakyembe amezindua rasmi makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria yaliopo mkoani Dodoma katika viunga vya Chuo Kikuu cha Dodoma baada ya wizara hiyo na watumishi wake 31 kuhamia rasmi makao makuu ya Serikali mkoani Dodoma.

Baada ya uzinduzi huo Mhe. Mwakyembe alisema kitendo cha kuhamia mkoani DODOMA ni utekelezaji wa agizo la kuhamia makao makuu ya Serikali ambalo lilitolewa mwezi Julai mwaka 2016 na hivyo watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao na kuwahudumia wananchi kama walivyokuwa Dar es salaam.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma, Mkuu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kanda ya Dodoma, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dodoma, Prof Kikula na watumishi 31 wa wizara ambao wamehamia Dodoma katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa agizo hilo la Serikali.

Awamu ya Kwanza yenye watumishi 31 wa wizara wakiongozwa na Waziri Dkt Dkt. Harrison Mwakyembe, Katibu Mkuu Prof. Sifuni Mchome na Naibu Katibu Mkuu Bw. Amon Mpanju imehamia rasmi mkoani Dodoma. Awamu ya pili na ya tatu zitafuata utaratibu ambao umewekwa na zoezi hilo linatarajiwa kukamilika mapema mwaka 2018.

Kufuatia kuhama rasmi kwa ofisi za wizara sasa mawasiliano yote yatafanywa kupitia anuani ya Katibu Mkuu Sanduku la Posta 315 Dodoma, namba ya simu ni 026 2321680, nukushi ni 026 2321679 na baru pepe ni ile ile ya This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it

Matukio Mapya

Hakuna Tukio kwa sasa.

Anuani

KATIBU MKUU

  • Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria,
  • Barabara ya Mkalama,
  • Jengo la Taaluma Na. 1,
  • Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria cha Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM,
  • S.L.B. 315,
  • DODOMA.
  • Simu:+255 26 2321680
  • Nukushi: +255 26 2321679
  • Tovuti www.sheria.go.tz
  • Barua pepe: km@sheria.go.tz