Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

ARDHI YA TANZANIA NI YA UMMA NA SIO YA MTU BINAFSI- DKT. NDUMBARO

Imewekwa: 31 Jan, 2023
ARDHI YA TANZANIA NI YA UMMA NA SIO YA MTU BINAFSI- DKT. NDUMBARO

Sheria ya Ardhi namba 4 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1999 na kuanza kutumika rasmi mwezi Mei mwaka 2001 zinaelekeza kwamba ardhi ni mali ya umma na imekabidhiwa kwa Rais kwa niaba ya Watanzania wote na si mali ya mtu binafsi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamishna wa Tume ya Afrika ya Haki za Watu na Binadamu Bi. Ourveena Geresha Topysonow na Dkt. Litha Musyimi Ogawa mwishoni mwa mwezi Januari, 2023 Jijini Dodoma.

"Ardhi ni ya wote na sio ya mtu binafsi hivyo jamii inapaswa kufuata maelekezo ya matumizi ya ardhi husika". Alisema Dkt. Ndumbaro.

Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa watu wanaoishi kwenye hifadhi lazima waelewe yanayokatazwa kufanyika humo ikiwemo kilimo na ufugaji.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana ambaye amehudhuria mkutano huo amesema kila mwananchi ana haki ya kumiliki ardhi na ili hilo liweze kutimia inabidi mwananchi huyo aishi sehemu ambayo anaweza kumiliki ardhi na hivyo hiyo ndiyo moja ya sababu ya kuhamisha wananchi kutoka Ngorongoro na kuhamia Msomera.

Awali wakieleza nia ya kutembelea Tanzania Makamishna hao wameeleza kuwa wametembelea Ngorongoro, Loliondo na Msomera ili kuona namna haki za Binadamu zilivyotekelezwa katika zoezi la kuhamisha wananchi kutoka Ngorongoro na kuhamia Msomera.

Makamishna hao wamesema wameongea na viongozi na wananchi wa maeneo hayo na kujionea hali halisi na kuishauri Serikali kuwa wazi na kujibu maswali yanayoulizwa kuhusu Ngorongoro ili kuondoa sintofahamu, kutenda haki na kutotumia nguvu kutekeleza zoezi hilo.

Mawaziri wengine waliohudhuria mkutano huo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stegolena Tax, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula na Naibu wake Mhe. Ridhiwani Kikwete.

Makamishna hao kabla ya kukutana na Mawaziri walifanya mazungumzo na viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Chama cha Wanasheria Tanganyika na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.