Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini ilinzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali, Executive Agencies Act, Cap.245. Kuanzishwa kwa Wakala kulitangazwa katika Gazeti la Serikali kwa Tangazo Namba 397 la tarehe 12 Disemba, 2005 na kuzinduliwa rasmi tarehe 23 Juni, 2006.
Wakala ilirithi kazi zote zilizokuwa zikifanywa na Idara ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali pamoja na zile za Msajili Mkuu. Wakala ulianzishwa kwa madhumuni ya kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
DIRA
Chanzo cha kuaminika katika utoaji wa taarifa za usajili wa matukio muhimu ya binadamu, ufilisi na huduma za udhamini.
DHIMA
Kulinda haki za wote kwa kutoa huduma bora za usajili wa matukio muhimu, ufilisi na udhamini ili kufanya maamuzi sahihi.
MAADILI YETU YA MSINGI
1. WELEDI
Tunatumia ujuzi na njia za kitaalam kuhakikisha tunatoa huduma zilizo bora
2. UADILIFU
Tunazingatia kanuni za maadili katika kutekeleza majukumu na kazi zetu, ili kuhakikisha uthabiti katika utendaji wetu.
3. KUMJALI MTEJA
Tunatoa huduma bora za kutegemewa na kuaminika kwa wakati ili kukidhi matarajio ya wateja wetu.
4. UZALENDO
Tunalinda maslahi ya taifa na si maslahi binafsi bila kujali changamoto zinazojitokeza katika utoaji huduma.
5. UBUNIFU
Tunazingatia ubunifu, uzoefu na ujuzi unaofaa ili kutoa huduma bora kwa wateja wetu.
6. USHIRIKIANO
Tunafanya kazi kwa ushirikiano, kujituma kwa kutambua uwezo na nguvu kazi tuliyonayo katika kutoa huduma bora
MAJUKUMU YA RITA:
Wakala unatekeleza majukumu yafuatayo:
i. Kusajili Vizazi na Vifo na kutoa vyeti vya Vizazi na Vifo;
ii. Kutayarisha takwimu za vizazi na vifo, Ndoa na Talaka;
iii. Kusimamia Mirathi baada ya kuteuliwa na Mahakama;
iv. Kutoa Leseni za kufungisha ndoa kwa viongozi wa dini mfano Mapadri, Wachungaji na Mashekhe;
v. Kutoa vibali maalumu vya kufunga ndoa bila kutangaza siku 21;
vi. Kutoa vibali ili kuruhusu ndoa ifungwe mahali maalumu mfano katika Hoteli, Hospitali, na hata kama watahitaji kufunga ndoa mahali pengine popote zaidi ya hizo zilizotajwa;
vii. Kusajili Ndoa na Talaka na kutoa nakala za shahada za ndoa na Talaka;
viii. Kutoa shahada ya kutokuwepo na pingamizi la kufunga ndoa kwa raia wa Tanzania anayetaka kufunga ndoa nje ya nchi;
ix. Kusajili na kutoa hati ya Usajili kwa Wadhamini wa Vyama vya siasa, Vikundi, Makanisa, Misikiti,watu binafsi,vyama vya michezo na vikundi mbalimbali vya kijamii;
x. Kusajili watoto wa kuasili na kutoa Hati za kuasili;
xi. Kusimamia Mali isiyokuwa na mwenyewe au ya watu walio chini ya umri wa utu uzima (chini ya miaka 18);
xii. Kufanya shughuli za ufilisi na upokezi rasmi;
xiii. Kusajili Makubaliano (Deeds of Arrangement);
xiv. Kuendesha mashauri ya mirathi, ufilisi na udhamini mahakamani;
xv. Kutayarisha na kuhifadhi wosia.
SHERIA ZINAZOSIMAMIA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA RITA
- Sheria ya Kabidhi Wasii Mkuu, Sura 27;
- Sheria ya Kuandikisha Vizazi na Vifo, Sura 108;
- Sheria ya Ndoa, Sura 29;
- Sheria ya Usajili wa Wadhamini, Sura 318;
- Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009;
- Sheria ya Mdhamini wa Serikali, Sura 31;
- Sheria ya Makampuni ya Mwaka 2002; na
- Sheria ya Usajili wa Makubaliano, Sura ya 26.
ANUANI YA OFISI
Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu,
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA),
Jengo la RITA, 4 Mtaa wa Simu/Makunganya,
S.LP. 9183,
11103 Dar es Salaam. Tanzania.
Simu: +255(22) 2924180/81
Nukushi: +255(22) 2924182
Barua pepe: info@rita.go.tz/ barua@rita.go.tz
facebook. com/ritatanzania
instagram.com/ritatanzania
twitter.com/ritatanzania
Tovuti: www.rita.go.tz
Piga Simu Bure: 0800 117 482