Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tume ya Kurekebisha Sheria

1.0 UTANGULIZI

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ni idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Wizara ya Katiba na Sheria. Tume imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Sura ya 171, na ilianza kazi rasmi tarehe 21 Oktoba, 1983.  Kwa mujibu wa sheria, Tume ina jukumu la kufanya mapitio ya sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ziandane na mazingira ya wakati uliopo kwa maendeleo endelevu.

2.0 MUUNDO WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA

Tume ya Kurekebisha Sheria inaundwa na Mwenyekiti na Makamishna wa Muda wawili. Tume ina Katibu ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za kila siku.

Mwenyekiti, Makamishna na Katibu huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tume ina vitengo nane ambavyo ni Mapitio ya Sheria, Utafiti na Elimu ya Sheria kwa Umma. Vitengo vingine ni Utawala na Rasilimaliwatu, Mipango na Uratibu, Uhasibu, Ukaguzi wa Ndani, Ugavi na Ununuzi. Vitengo hivi vinafanya kazi chini ya uongozi wa Katibu Mtendaji wa Tume.

3.0 DIRA

Kuwa taasisi inayoaminiwa kwenye maboresho ya Sheria ili kukuza utawala wa sheria kwa maendeleo ya jamii.

4.0 DHIMA

Kufanya mapitio na utafiti ili kuboresha sheria za Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania kulingana na misingi ya Katiba kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

5.0 MAJUKUMU YA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA

Majukumu ya Tume kama yalivyoainishwa katika kifungu cha 4 (1), (2) na (4) cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Sura ya 171 ni kufanya mapitio, utafiti na kutathmini maeneo au mfumo wa sheria husika na kutoa mapendekezo kwa lengo la kuiboresha.

Kifungu cha 4 (1), (2) na (4) cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Sura ya 171, kinaainisha majukumu mahususi ya Tume kuwa ni:

  a)  Kuchunguza sheria yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuiendeleza na kuiboresha;

  b)  Kupitia sheria au tawi la sheria na kupendekeza hatua muhimu ili;

          i. Kuifanya sheria hiyo iendane na mazingira ya sasa ya Tanzania.

         ii. Kuondoa kasoro au upungufu mwingine katika sheria;

        iii. Kufuta sheria zilizopitwa na wakati au sheria zisizohitajika;

         iv. Kuunganisha sheria zinazohusiana na kufanywa sheria moja (Consolidation) na;

         v. Kuweka sheria au sehemu ya sheria katika uandishi ulio sahihi na rahisi;

 c)  Kupendekeza njia bora za usimamizi wa sheria na utolewaji haki;

  d) Kufanya tathmini ya utekelezaji wa Sheria;

 e) Kwa kuelekezwa na Waziri wa Katiba na Sheria au Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushauri au msaada wa kisheria  kwa wizara, idara ya umma au taasisi kwa kufanya mapitio ya sheria yoyote na kutoa mapendekezo ya marekebisho ili kuendana na mazingira ya sasa na;

  f) Kwa kuombwa, kutoa ushauri au maelezo kwa Kamati ya Makatibu Wakuu kuhusu mapendekezo ya utungwaji wa sheria ili kuhakikisha maendeleo sawia ya sheria katika nchi.

Ili kutekeleza Majukumu haya, Tume inaweza:-

     i. Kuanzisha mfumo wa ushirikiano au kufanya kazi pamoja na watu wa ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano;

    ii. Kuweka mfumo wa kupata taarifa kutoka nchi nyingine zinazohusiana na mifumo ya sheria ambayo inaweza kuifanya Tume kurahisisha kazi zake;

   iii. Kuchapisha au kufanikisha kuchapishwa kwa masuala yanayohusiana na urekebishaji sheria wa nchi nyingine;

    iv.  Kuitisha au kufanikisha kuitishwa semina, mihadhara au mikutano yoyote kwa lengo la kujadili au kutoa habari au masuala yanayohusiana na urekebishaji wa sheria Tanzania.