WADAU WA HAKI JINAI WATAKIWA KUWEKEZA MATUMIZI YA AKILI UNDE KUBORESHA UPATIKANAJI WA HAKI
Wadau wa mfumo wa Haki Jinai nchini wametakiwa kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kidijitali, hususan Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), ili kurahisisha michakato ya utoaji haki na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa haraka na kwa wakati.
Wito huo umetolewa na Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Manyara, Dkt. Adam Mambi, mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo ya siku tatu kuhusu kuimarisha upelelezi na uendeshaji wa mashauri kwa wadau wa mfumo wa Haki Jinai, yaliyofanyika katika ukumbi wa Lush Garden Hotel jijini Arusha.
Dkt. Mambi ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yamekuwa fursa muhimu ya kuwaunganisha wadau wa mfumo wa Haki Jinai na kujenga ushirikiano katika kuimarisha upatikanaji wa haki.
Aidha, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa wa pamoja katika kupambana na uhalifu wa kidijitali pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Joseph Michael, mshiriki kutoka Kampuni ya Vodacom, ameishukuru Wizara kwa kuandaa mafunzo hayo akieleza kuwa maarifa waliyoyapata yatakuwa na manufaa kwa wananchi kupitia kuboreshwa kwa huduma za haki.
Naye Neema Ulamba, Hakimu Mkazi kutoka Mahakama ya Arusha, amesema mafunzo hayo yatamsaidia kuimarisha uwezo wa kuchunguza, kuchakata na kutathmini vielelezo kwa wakati, jambo litakaloongeza ufanisi katika utendaji wa mahakama na kufanya maamuzi kwa kuzingatia ushahidi na misingi ya sheria.
Mafunzo hayo yanaendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza matumizi ya teknolojia katika kuharakisha maendeleo ya Taifa, ikiwemo matumizi ya Akili Unde katika kuboresha utoaji wa huduma.