Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Chana Awasilisha Taarifa ya Utekelezaji Majukumu ya Wizara Kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge

Imewekwa: 22 Jan, 2024
Dkt. Chana Awasilisha Taarifa ya Utekelezaji Majukumu ya Wizara Kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge

Na George Mwakyembe - WKS Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Pindi Chana amewasilisha taarifa ya utakelezaji   wa majukumu ya Wizara kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria. Taarifa zilizowasilishwa ni taarifa ya majukumu ya Mahakama pamoja na taarifa inayohusu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Mhe. Balozi Chana amewasilisha taarifa hiyo leo tarehe 22 Januari, 2024 jijini Dodoma kwa kuwashukuru wajumbe wa kamati pamoja na Mwenyekiti kwa ushirikiano wanaotoa katika kutekeleza majukumu ya Wizara pamoja na Taasisi zake.

Akiongea kwenye kikao hicho Mhe. Chana amesema “Nawashukuru sana wajumbe mmekuwa mbele kutupa ushauri, lakini pia mmekuwa mkitoa ushirikiano mzuri pale tunapokuwa tunahitaji ushauri wenu, leo tutawasilisha ripoti mbili ya Mahakama na ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.”

Naye Mtendaji Mkuu wa Mhakama Prof. Elisante Ole Gabriel ameleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 Mahakama wametenga bajeti ya kununua magari sita yatakayo toa huduma ya Mahakama inayotembea (Mobile Court) ili kuwafikia wananchi wengi katika kutatua kesi za jinai pamoja na kesi za madai.

Pia Ole Gabriel amesema “Mahakama ina magari mawili tu ambayo yamekuwa yakitoa huduma ya Mahakama inayotembea (Mobile Court) ambayo yapo katika mkoa wa Dar es salaam na Mwanza lakini bado magari hayatoshi”

Aidha, Ole Gabriel ameongeza kuwa Mahakama pia imetengeneza mfumo wa kuendesha kesi kidigitali e-CMS (Electronic Case Management System) ambao utarahisisha uendeshaji wa kesi mbalimbali pasipo kuchelewesha kesi.

Kwa upande mwingine Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Mohamed Hamad amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume na kufafanua kuwa Tume imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kwa makosa yanayofanywa kinyume na haki za binadamu pamoja na kuwachukulia hatua wale wote wanaofanya makosa hayo.

Mhe. Hamad amesema “kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Tume imepokea malalamiko mengi yanayohusu migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo tayari imeishafanyiwa kazi na kutolewa mapendekezo namna ya kutatua.

Akihitimisha, Mhe. Balozi Chana amewashukuru wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria na kuwaahidi kuwa Wizara na taasisi zake imepokea mapendezo namna ya kuboresha utendaji kazi katika kuhakikisha Wizara inaendelea kutatua kero za wananchi.