Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

DKT. HOMERA AIPONGEZA OFISI YA MWANASHERIA MKUU KWA UTENDAJI MAHIRI

Imewekwa: 28 Apr, 2026
DKT. HOMERA AIPONGEZA OFISI YA MWANASHERIA MKUU KWA UTENDAJI MAHIRI

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa utendaji wake mahiri na mchango wake katika kuhakikisha Serikali inapata ushauri wa kisheria kwa wakati na kwa ufanisi, hususan katika usimamizi na uchambuzi wa mikataba.

Akizungumza Aprili 28, 2026 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Watumishi wa Ofisi hiyo, Dkt. Homera ameeleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kuwa kiungo muhimu katika uendeshaji wa Serikali kutokana na jukumu lake la kikatiba la kuwa mshauri mkuu wa masuala yote ya kisheria.

Aidha, Dkt. Homera ameeleza kuridhishwa kwake na hatua ya kuunganisha mfumo wa kisasa wa TEHAMA, Mfumo wa Serikali wa Ununuzi wa kielektroniki (NeST) na mfumo wa OAG-MIS wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akibainisha kuwa hatua hiyo italeta mapinduzi makubwa katika mchakato wa upekuzi na uchambuzi wa mikataba ya Serikali ambapo utaongeza kasi, uwazi na ufanisi katika kushughulikia nyaraka za kisheria

“Matumizi ya mifumo ya kidijitali kama NeST na OAG-MIS yanaonesha dhamira ya Serikali ya kujenga taasisi zinazokwenda na wakati, jambo lilosaidia kuongeza tija, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali yao,” amesisitiza Dkt. Homera

Aidha, Dkt. Homera amesema kuwa Ofisi ya Mwanansheria Mkuu wa Serikari ina nafasi kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya miaka 25, akihimiza watumishi wake kuendelea kujiendeleza kitaaluma na kuongeza ujuzi ili waweze kutoa ushauri bora wa kisheria utakaoendana na mahitaji ya uchumi wa kisasa.