Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Ndumbaro Aongoza Kikao cha Majadiliano cha Mchakato wa Katiba Mpya

Imewekwa: 29 Aug, 2023
Dkt. Ndumbaro Aongoza Kikao cha Majadiliano cha Mchakato wa Katiba Mpya

Na George Mwakyembe na Lusajo Mwakabuku - WKS

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameongoza Kikao cha Mawaziri wa Sheria na Wanasheria Wakuu wa Serikali Wastaafu na waliopo madarakani kuhusu Majadiliano ya Mchakato wa Katiba Mpya pamoja na Mkakati wa Elimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho tarehe 28 Agosti, 2023 Jijini Dar es salaam Dkt. Ndumbaro amesema lengo la kikao hicho ilikuwa ni kujadili mchakato wa Katiba Mpya pendekezwa ulioanza mwaka 2014 ambao bado haujafikia muafaka.

Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa kikao hicho kimelenga kuongeza uelewa na kutoa elimu juu ya Mwenendo wa Mchakato wa Katiba Mpya.

"Wizara kwa kutambua baadhi ya wananchi kudai Katiba Mpya, uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Utawala unaozingatia Haki za Msingi za Binadamu na mambo mengine mengi ambayo yanahusisha shughuli za kimaendeleo na Siasa katika nchi. Kutokana na kuongezeka kwa hoja hizo na viashiria vya jamii kutofahamu haki zao Kikatiba, baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi, kushindwa kuheshimu utawala wa sheria na kutokujua wajibu wao kwa Taifa, hali inayopelekea kuwepo kwa mahitaji ya kuweka mwongozo wa utoaji wa elimu ya Katiba katika masuala ya Haki za Binadamu na Haki na wajibu kwa jamii ya Watanzania katika ngazi zote za kiutawala," amesema Waziri Dkt.  Ndumbaro.

Dkt. Ndumbaro alifafanua baadhi ya majukumu ya Wizara kwenye kikao hicho kuwa   ni Kuratibu mchakato wa Katiba ya Mwaka 1977 kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wakiwemo Mawaziri Wastaafu, Wanasheria na wale waliopo madarakani kupata mrengo mmoja uliokusudiwa.

"Nimefungua kikao hiki leo ili kupitia kikao hiki tupate maoni yenu kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara kufahamu wapi kulitakiwa kufanyiwa marekebisho Katiba ya mwaka 1977." Ameongeza Dkt. Ndumbaro.