Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

DKT. NDUMBARO AZINDUA KITABU CHA MIAKA 60 YA UHURU NA SEKTA YA SHERIA

Imewekwa: 08 Feb, 2023
DKT. NDUMBARO AZINDUA KITABU CHA MIAKA 60 YA UHURU NA SEKTA YA SHERIA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amezindua Kitabu cha Miaka 60 ya Uhuru na Sekta ya Sheria Tulipotoka, Tulipo na Tunapokwenda Tangu Mwaka (1961 - 2021), uzinduzi huo umefanyika tarehe 07 Februari, 2023 Jijini Dododma.

Kitabu hicho chenye Sehemu nne na Sura 18 kimebeba maudhui kuhusu Sekta ya sheria kikieleza mambo yaliyofanyika katika Sekta ya sheria kwa miaka 60 tangu Tanzania Bara kupata uhuru.

Akiongea kwenye uzinduzi Mhe. Ndumbaro amesema “Kitabu hiki kimebainisha changamoto pamoja na mafanikio katika sekta ya sheria kwa kipindi cha miaka 60 ya uhuru, hivyo  ni hazina kwa vizazi vijavyo kusoma ili kuelewa masuala ya sheria.”

Naye Prof. Kabudi ambaye ni moja wa watunzi wa kitabu hicho amesema kwa miaka mingi historia ya Tanzania imekuwa ya simulizi badala ya kuandikwa, hivyo kupitia kitabu hicho watu wengi watafaidika kuelewa kiundani kuhusu nchi ilipotoka, ilipo na kupata tathmini ya inapoelekea  na kufanya vijana wengi wa sasa na baadaye kujua jinsi nchi ilivyopiga hatua ya maendeleo katika sekta ya sheria  na sekta zingine.

Kwa upande wake Prof. Sifuni Mchome ameshauri kitabu hicho kuendelea kutolewa katika toleo jipya kila baada ya miaka mitano. "Kitabu hiki kitakuwa kinatoka kwa matoleo na hili ni Toleo la Kwanza la miaka 60 na kila baada ya miaka mitano litolewe Toleo la jipya nia na madhumuni ni kuendelea kukumbusha historia ya nchi yetu kwa vizazi na vizazi," amesema Prof. Mchome.