DKT. TULIA APONGEZA MAFUNZO YA SAMIA LEGAL AID JIJINI MBEYA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendesha mafunzo ya elimu ya Msaada wa Kisheria kwa baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa Jijini Mbeya
Dkt. Tulia ametoa pongezi hizo Mei 23, 2025 alipokua anafunga mafunzo hayo katika viwanja vya Shule ya Msingi Asanga ambapo amesema kuwa elimu hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa viongozi hao, kwani imewaongezea uelewa na utashi katika utatuzi wa Changamoto za wananchi katika maeneo yao.
Aidha, Dkt. Tulia amewasilisha salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa mpango huu wa Samia Legal Aid ni sehemu ya jitihada za Rais kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria na elimu ya haki zao bila vikwazo.
Ameomba mafunzo hayo yawe endelevu kwa kuwa wananchi wameyaelewa na kuyapokea kwa moyo wa shukrani.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria , Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, amewapongeza wataalamu waliotoa elimu hiyo kwa umahiri na kujitolea kwao kuhakikisha wananchi wa Mbeya wanapata uelewa sahihi wa masuala ya kisheria.
Mhe. Ndumbaro amesema elimu hiyo imelenga kutatua migogoro ya kijamii kwa Njia mbadala , kukuza utawala bora, na kuandaa jamii yenye uelewa wa masuala ya uchaguzi.
Amewasihi wananchi kuendeleza amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu, huku akiahidi kuwa Wizara yake itaangalia uwezekano wa kuendeleza mafunzo hayo kwa mikoa mingine nchini.