ELIMU YA KISHERIA YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA VYUO VIKUU
Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Idara ya Huduma za Msaada wa Kisheria, imeendelea kutoa elimu ya kisheria kwa umma ikiwemo jinsi ya kujikinga na ukatili wa kijinsia pamoja na namna ya kuwasaidia wahanga wanaopitia ukatili huo.
Akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) Mkoani Dodoma, 28 Aprili, 2026, wakati wa mdahalo wa vyuo vikuu, Dkt. Geofrey Chambua amesema kuwa Wizara imetambua umuhimu wa kundi hili la vijana kupewa elimu juu ya haki zao na namna ya kujilinda dhidi ya matukio ya kikatili.
‘’Vitendo vya ukatili vimekuwa vikijitokeza kwa sura tofauti hali inayosababisha hofu, msongo wa mawazo na hata kuathiri maendeleo ya kijami, kwa ktambua umuhimu wa vijana Wizara imeona ni muhimu kutoa elimu hii inayolenga kuwajengea uwezo wa kutambua viashiria vya unyanyasaji mapema na kuchukua hatua stahiki kabla madhara hayajawa makubwa’’ alisema Dkt. Chambua.
Dkt. Chambua pia alieleza kuwa ukimya wa wahanga umekuwa ukichochea kuendelea kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na ni muhimu vijana kujenga utamaduni wa kuzungumza na kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo.
Aidha Dkt. Chambua alifafanua mbinu mbalimbali za kujikinga na unyanyasaji, ikiwemo kuwa na uelewa wa mipaka binafsi, kuepuka mazingira hatarishi, na kuhakikisha wanakuwa na marafiki au watu wa kuaminika wanapokuwa katika mazingira mapya.
Naye Mkurugenzi wa TEHAMA Kutoka Mahakama kuu ya Tanzania, Bw. Enock Kalege, alisisitiza matumizi sahihi ya teknolojia, hasa mitandao ya kijamii, ambayo wakati mwingine hutumika kama njia ya kuwanyanyasa watu.
Bw. Kalege alieleza taratibu za kutafuta msaada wa kisheria pindi wanapokumbana na ukatili na kusema kuwa kuna taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za msaada wa kisheria bure, na kwamba ni haki ya kila mwanafunzi/kijana kupata msaada huo bila ubaguzi.
Kwa upande wake, Meneja wa Chuo Cha CBE kampasi ya Dodoma, Dkt. Liberatus Gabagambi, ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuhakikisha elimu ya kisheria inawafikia vijana katika taasisi za elimu ya juu na kuratibu kampeni mbalimbali zinazolenga kuijua sheria, haki na wajibu ili kupunguza vitendo vya ukatili na kuleta haki na usawa kwa wote.