Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

ELIMU YA  KISHERIA  YAPATA MSUKUMO  CHANYA WA VIJANA

Imewekwa: 28 Apr, 2026
ELIMU YA  KISHERIA  YAPATA MSUKUMO  CHANYA WA VIJANA

Serikali imeendelea kuyafikia makundi mbalimbali wakiwemo   vijana  kufuatia ushiriki wao katika mdahalo uliolenga kujadili namna wanavyoweza kuchochea upatikanaji wa huduma za kisheria, kutambua haki, wajibu  na upatikanaji wa huduma za Msaada wa Kisheria kwa wananchi bila malipo.

Hayo yamebainishwa na  Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria  Bi. Ester Msambazi, wakati wa  mdahalo uliowakutanisha wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Mawakili wa Serikali, wataalam wa TEHAMA  na Wataalam wa masuala ya kijamii.

“Tunataka vijana wapate uelewa wa kutosha juu ya masuala ya kisheria ili waweze  kufahamu namna bora ya kuweza kufanya pindi wanapokutana na mambo yanayohitaji Msaada wa Kisheria.Aidha, kuhakikisha tunapata mabalozi wazuri wa elimu ya kisheria kwa jamii zinazowazunguka.Alisema Msambazi.

Katika hatua nyingine, Amidi wa Shule Kuu ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Elia Mwanga, amesema kuwa ushiriki wa vijana  ni hatua muhimu  katika kuleta uelewa wa pamoja  na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.Alibainisha kuwa kupitia majukwaa ya elimu,mitandao ya kijamii na shughuli za kijamii vijana  wanapata fursa ya kutoa maoni yao yatakayowezesha kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu ya kisheria katika maeneo mbalimbali kutokana na jiografia ya maeneo  wanapotoka.

Wakizungumza katika nyakati tofauti tofauti baadhi ya vijana walioshiri kutoka chuoni hapo wamepongeza kuanzishwa kwa jukwaa hilo, wakisema limewapa mwanga kuhusu masuala ya kisheria sambamba na upatikanaji haki.

Wizara imeendelea kutumia mbinu mbalimbali katika kuhakikisha elimu ya kisheria inaifikia jamii ikiwa ni pamoja na majukwa ya elimu yatakayowezesha vijana kuwa mabalozi wa haki,yakihimiza matumizi ya teknolojia na mbinu bunifu katika kufikisha elimu ya kisheria kwa wananchi