HAKI KWA WANANCHI SIYO HUDUMA YA HIARI NI WAJIBU WA MSINGI WA SERIKALI
Wizara ya Katiba na Sheria inatarajia kuanza utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria Awamu ya Pili kwa lengo la kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mtanzania kwa wakati na usawa bila ubaguzi wa eneo, kipato ama hali ya kijamii.
Akizungumza Bungeni wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili siyo tu mpango wa kawaida wa utoaji huduma, bali ni mageuzi ya msingi ya mfumo wa haki nchini.
“Kupitia utekelezaji wa Kampeni hii, tunaweka msingi wa Taifa lenye haki, usawa na utulivu, ambapo sheria inakuwa nguzo ya mshikamano wa kitaifa na chachu ya maendeleo endelevu” Amesema Dkt. Homera.
Aidha, Mhe. Homera amesema kuwa kupitia Kampeni hii, Wizara inajenga mfumo jumuishi, unaofikiwa na wananchi wote, unaounganisha Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wadau wa Maendeleo, na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika kupata haki.
“Nitoe wito kwa Watendaji wote wa Serikali kuelewa na kuishi dhamira hii ya kitaifa kwamba; haki kwa wananchi siyo huduma ya hiari ni wajibu wa msingi wa Serikali, na hivyo utekelezaji wa MSLAC II utasimamiwa na ngazi zote za serikali kwa uwajibikaji, weledi na matokeo yanayopimika, ili kuimarisha utawala wa sheria, amani na maendeleo ya Taifa letu kuelekea DIRA 2050” amesisitiza Dkt. Homera.
Pia amesema kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inachukua hatua ya kihistoria na ya kimapinduzi katika kujenga mfumo wa haki unaowafikia wananchi wote.
“Tunadhamiria kwa dhati kugeuza msaada wa kisheria kutoka kuwa huduma ya hiari kwenda kuwa haki ya msingi ya kila Mtanzania, bila kujali mahali alipo au hali yake ya kiuchumi”.
Pamoja na hayo amesema kuwa hatua hiyo inaweka msingi imara wa utekelezaji wa DIRA 2050, kwa kutambua kuwa hakuna maendeleo ya kweli bila upatikanaji wa haki kwa wote.