Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kamati ya Bunge Yakagua Mradi wa Ujenzi wa IJC Njombe

Imewekwa: 14 Mar, 2024
Kamati ya Bunge Yakagua Mradi wa Ujenzi wa IJC Njombe

Na Lusajo Mwakabuku – WKS, Njombe.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria tarehe 13 Machi, 2024 imekagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki IJC kinachojengwa mkoani Njombe chenye thamani ya shilingi takribani Bilioni 7.6 mradi unaotekelezwa na Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa zoezi la ukaguzi wa kituo hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Kizito Mhagama amesema mradi huo ni moja ya miradi mikubwa inayotekelezwa nchini kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na Mtekelezaji wa mradi ni Mhimili wa Mahakama.

“Mradi huu ni wa kutoa huduma za sheria kwenye jengo moja ‘Integrated Justice Centre’ ambapo Mahakama za ngazi mbalimbali zinakuwa katika jengo moja ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi lakini pia wanaotoa haki waweze kutekeleza wajibu wao na majukumu yao kwa namna ambayo ni jumuishi na rahisi zaidi,” ameeleza Mhe. Dkt. Mhagama na kuongeza kuwa;

“Hii ni hatua kubwa sana ya kuboresha mifumo ya utoaji haki nchini ikizingatiwa kwamba, tunaendelea kuijenga Tanzania ambayo ina hali ya utulivu na amani ya kutosha,” amesema Mhe. Mhagama.

Aidha, Mhe. Dkt. Mhagama amesema kuwa, kwakuwa mradi huo umeshuhudiwa na Wabunge wa Kamati hiyo kwa pamoja ni imani yao kuwa changamoto zozote zitakazojitokeza zitatolewa taarifa kwa ukaribu zaidi ili wakati wa kupanga bajeti zisaidie kutatuliwa kwa mwaka ujao wa fedha ambao utahusu pia uendelezaji na ujenzi wa miundombinu ya utoaji haki kwa Watanzania.

Kamati imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuthubutu na kwa kuamua kwa dhati kabisa kusogeza huduma ya utoaji haki kwa wananchi wa Tanzania ambao wanahitaji huduma hiyo inayotekelezwa mkoani Njombe na maeneo mengine nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema ukaguzi huo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria unaenda sambamba na maelekezo ya Rais Samia ya kuboresha miundombinu ya utoaji haki kwa maana ya “Reforms & Rebuilding” ili Watanzania wote wapate haki kwa usawa na kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

“Kamati hii ya Bunge inatusaidia sana mawazo na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha shughuli za utoaji haki kupitia Serikali na Mahakama. Tunajua jukumu la Bunge ni kupitisha bajeti, kutunga sheria na kuisimamia Serikali, hivyo leo tupo katika jukumu mojawapo la Bunge la kusimamia Serikali ‘Oversight role’ ya kupitia Kamati ya Bunge baada ya kupitisha Bajeti hii ndiyo kazi ya Kamati,” amesema Mhe. Dkt. Chana.

Mhe. Dkt. Chana amesema, Wizara ya Katiba na Sheria imedhamiria kuhakikisha utawala wa sheria unakuwa ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali.

“Tunataka kuona wawekezaji wanakuwa na imani na Utawala wa Sheria, tunataka Watanzania waishi kwa amani, kwa uhuru bila kuwepo na changamoto za kijinai na pale zinapojitokeza basi tuwe na miundombinu ya kudhibiti na kukabiliana nazo,”

Mhe. Dkt. Chana ameongeza kuwa miundombinu hiyo inayojengwa inakwenda sambamba na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia Duniani hasa katika eneo la utoaji haki, ikiwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa IJC Njombe.

Naye, Mkadiriaji Majengo kutoka Mahakama ya Tanzania, Bw. Abdallah Nalicho akifanya wasilisho fupi la Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Njombe, amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho umezingatia mahitaji mbalimbali yanayoendana na uhalisia na matarajio ya wananchi watakaopata huduma za haki ndani ya jengo hilo. Matarajio hayo ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri, kuokoa muda na kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa watoa haki.

“Mathalani usanifu wa jengo hili umezingatia mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum mfano; walemavu, watoto, akina mama wanaonyonyesha na wajawazito, wazee wasiojiweza na wadau mbambali katika mnyororo wa utoaji haki wanaosaidiana na Mahakama (Waendesha Mashtaka, Mawakili wa kujitengemea, Watoa ushauri wa kisheria, Ustawi wa Jamii, Dawati la jinsia na Mahakama maalum kwa ajili ya watoto waliokinzana na Sheria,” ameongeza Bw. Nalicho.

Akielezea faida za ziada za ujenzi wa Kituo hicho, Bw. Nalicho amesema kimesaidia kutoa ajira kwa wataalum wa masuala ya ujenzi wapatao 23 na wafanyakazi wasio wataaluma wa ujenzi wenyeji wa Mkoa wa Njombe na hivyo kukuza na kuongeza kipato cha wananchi kupitia Mradi huo.