Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

KAMPENI YA MAMA SAMIA YAWAFIKIA WAFUNGWA 12,000 HUKU MAHABUSU 6900 WAKIACHIWA

Imewekwa: 10 Jun, 2025
KAMPENI YA MAMA SAMIA YAWAFIKIA WAFUNGWA 12,000 HUKU MAHABUSU 6900 WAKIACHIWA

Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza kutoka Jeshi la Magereza Nchini CP Nicodemus Tenga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwani imewezesha kupunguza mrundikano wa mahabusu na wafungwa magerezani.

“Kampeni hiyo iliyopewa jina la Mama Samia imewezesha wafungwa 12,000 kupata elimu na msaada wa kisheria huku mahabusu 6900 wakiachiwa kupitia msaada huo na hivyo kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa, awali mwaka 2021 wafungwa walikuwa 32,700 lakini takwimu za jana Juni 9, 2025 wamebaki wafungwa 26,896 pia uwiano wa wafungwa magarezani umekuwa asilimia 75 wafungwa na 25 mahabusu wakati zamani ilikuwa asilimia 50 wafungwa na 50 mahabusu.”, amefafanua CP Tenga.

CP Tenga ameyasema hayo leo Juni 10, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Cate Convection mjini Morogoro wakati wa Uzinduzi wa mafunzo yanayofanyika kwa muda wa siku tano kwa Maafisa Sheria na Maafisa Urekebu 170 wa Jeshi la Magereza Nchini ambapo mgeni rasmi alikua Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt Franklin Jasson Rwezimula aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi.