Kipaumbele ni Wilaya Ambazo Hazina Mahakama – Sagini

Na William Mabusi – WKS Dodoma
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amesema kipaumbele cha Serikali ni kujenga Mahakama kwenye Wilaya zote ambazo hazina Mahakama.
Mhe. Sagini ameyasema hayo leo Mei 24, 2024 Bungeni Dodoma alipokuwa anajibu swali la Mhe. Jonas Wiliam Mbunda Mbunge wa Mbinga Mjini aliyetaka kujua lini Serikali itajenga jengo la kisasa la Mahakama ya Wilaya ya Mbinga.
”Kulingana na ukubwa wa changamoto tulizonazo za uhaba na uchakavu wa majengo, kwa sasa, kipaumbele ni kujenga majengo ya Mahakama katika Wilaya ambazo hazina kabisa majengo ya Mahakama.” Alisema.
Mhe. Sagini amekiri kwamba jengo Mahakama ya Wilaya ya Mbinga siyo la kisasa. Hata hivyo, jengo hilo bado lina hali nzuri kwa kuwa limekuwa likifanyiwa ukarabati mdogo mara kwa mara. Aidha, huduma za kimahakama zinatolewa bila changamoto katika jengo hilo ambalo limeunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuwezesha utoaji wa huduma kupitia mifumo ya kielektroniki inayotumiwa na Mahakama ikiwemo uendeshaji wa mashauri.