Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MAAFISA 170 WA JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJENGEWA UWEZO MOROGORO

Imewekwa: 09 Jun, 2025
MAAFISA 170 WA JESHI LA MAGEREZA NCHINI WAJENGEWA UWEZO MOROGORO

Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza kutoka Jeshi la Magereza Nchini (CP) Nicodemus Tenga leo Juni 09, 2025 ameongoza mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa Sheria na maafisa Urekebu 170 kutoka vituo mbalimbali vya magereza Tanzania bara ambapo mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa siku tano katika ukumbi wa Cate Convention Centre Mjini Morogoro.

CP Tenga ameongoza majadiliano mbalimbali ya Kisheria pamoja na mapokezi ya wafungwa na hesabu za kifungo ikiwa ni siku ya kwanza ya mafunzo hayo ambapo mada nyingine watakazo jadiliana ni pamoja na huduma za Msaada wa Kisheria na adhabu mbadala.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Wakili Jane Lyimo amesema mafunzo hayo yanapaswa kuwajengea uwezo maafisa magereza hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa tija, usawa na haki.

Aidha Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Magereza Nchini ambapo uzinduzi rasmi utafanyika kesho Jumanne tarehe 10 Juni, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Chacha Maswi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa uzinduzi huo.