MAAFISA MAGEREZA WAASWA KUJIENDELEZA ILI KUBORESHA UTENDAJI KAZI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ally Senga Gugu ametoa wito kwa maafisa magereza wote nchini kujiendeleza ili waweze kuboresha utendaji kazi wao na kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwani mafanikio ya Jeshi la magereza yanategemea sana utekelezaji wa majukumu yao kwa weledi.
Gugu ameyasema hayo leo Juni 13, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Cate Convetion Centre Mjini Morogoro wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo maarisa sheria na maafisa urekebu wa Jeshi la Magereza 170 kutoka katika vituo vyote Nchini.
Amesema,” nimeambiwa kuwa mada za mafunzo zimehusu mapokezi ya wafungwa, hesabu za vifungo, huduma za wafungwa wa makundi maalumu, elimu kuhusu mikataba, adhabu mbadala, Huduma za msaada wa Kisheria kwa wafungwa na mahabusu, urekebu na utengamanisho wa wafungwa, rufaa na mapitio ya adhabu”.
Gugu ameongeza kuwa ni matarajio ya serikali kuwa mafunzo hayo yataongeza ufanisi wa maafisa magereza na kuboresha mfumo wa haki jinai nchini huku akipingeza ushirikiano baina ya Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi kuwa ni wa kuigwa kwani unawezesha ufanisi na mafanikio.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji Haki Wakili Jane Lyimo amesema Wizara ya Katiba na Sheria imeweza kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na ununzi wa vifaa 30 vya mahakama mtandao pamoja na kufanya tathmini katika magereza 4 ili kubaini sababu za msongamano wa wafugwa na mahabusu.
Wakili Lyimo ameongeza kuwa ushirikiano huu unaonesha namna ambavyo taasisi za serikali zinapaswa kufanyakazi kwa pamoja na kwa ushirikiano pia ameeleza kuwa Wizaya hiyo imepokea maoni na mapendekezo ya maeneo ya kuimarisha ushirikiano ili kuboresha mfumo wa haki jinai nchini.
Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza Tanzania Bara CP. Nicodemus Tenga amesema hadi sasa maafisa magereza waliopatiwa mafunzo hayo wamefikia 290 huku akiwaagiza maafisa hao kupeleka elimu waliyiopata kwa maafisa wenzao kupitia katika mabaraza ya maaskari.