MAAFISA MAGEREZA WAPONGEZWA KWA UADILIFU

Maafisa magereza Nchini wamepongezwa kwa kufanya kazi kwa uadilifu, kusimamia haki, kurekebisha tabia za wafungwa na kuendeleza utawala wa sheria hata katika mazingira yenye changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa rasilimali.
Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki, Wakili Jane Lyimo ametoa pongezi hizo leo Juni 10, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Cate Convection mjini Morogoro, wakati wa Uzinduzi wa mafunzo ya siku tano kwa Maafisa Sheria na Maafisa Urekebu 170 wa Jeshi la Magereza Nchini.
Mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo alikua Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin Jasson Rwezimula, aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi.
Wakili Lyimo amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kukuza ushirikiano baina ya maafisa sheria na maafisa urekebu, kuwawezesha kuzingatia haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao hata katika mazingira magumu pamoja na kujenga mfumo wa haki unaotenda kazi kwa ufanisi, uwazi na kwa kutumia ushahidi wa kisheria.
Wakili Lyimo aliongeza “Ninyi mnatekeleza jukumu muhimu katika kubadilisha maisha ya watu waliokosea, kazi yenu sio tu kuwaweka ndani bali kuwawezesha kutoka wakiwa bora kwa kuwapa mafunzo, ushauri nasaha na mazingira ya kujirekebisha" alisisitiza.
Aidha Wakili Lyimo ameongeza kuwa mafunzo hayo ni ya awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza ilifanyika mwezi Mei na ilihusisha maafisa 120 na sasa mafunzo yamejumuisha maafisa 170 na kufanya idadi ya maafisa urekebu na maafisa sheria wa jeshi la magereza nchini ambao wamejengewa uwezo kufikia 290