Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Maandalizi ya Kikao Cha 77 Cha Tume ya Haki za Binadamu na Watu Yaiva.

Imewekwa: 06 Oct, 2023
Maandalizi ya Kikao Cha 77 Cha Tume ya Haki za Binadamu na Watu Yaiva.

Na. Lusajo Mwakabu – WKS Arusha

Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wizara pamoja na Taasisi mbalimbali za Serikali inaendelea na maandalizi ya kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachotarajiwa kufanyika Jijini Arusha katika kumbi za AICC kuanzia tarehe 20 Oktoba mpaka tarehe 9 Novemba mwaka huu.

Akielezea hatua ya maandalizi ya Kikao hicho mbele ya Makatibu Wakuu kutoka Wizara zilizoalikwa na viongozi wengine wa Taasisi tarehe 06 Oktoba, 2023, Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo alisema hatua za maandalizi ya kikao hicho kinachotarajiwa kuwa na watu wasiopungua 700 yanaendelea vyema hasa kutokana na ushirikiano unaotolewa Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Fedha iliyopitisha fedha kwa ajili ya kikao hicho.

Aidha, Katibu Mkuu aliwaomba viongozi na watumishi waliohudhuria kikao hicho cha maandalizi kupitia taarifa ya kamati ya maandalizi kuiboresha ili iweze kuwasilishwa kwenye kikao cha Mawaziri na hatimaye kwa pamoja taifa liweze kufakinisha kikao hicho na kuleta tija kwa watanzania na waafrika kwa ujumla wake.

“Wizara ya Katiba na Sheria kama Wizara yenye kuratibu na kusimamia masuala ya Haki za Binadamu na Watu nchini, inaendelea na maandalizi ya Kikao cha 77 cha Kamisheni ya Haki za Binadamu na Watu kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyoelekeza. Mkutano huu unahusisha sekta mbalimbali zaidi ya masuala ya haki za binadamu na watu, yakiwemo masuala ya ushirikiano wa kimataifa; utamaduni, sanaa na michezo, fedha na uchumi, ulinzi na usalama, afya na habari na mawasiliano. Hivyo, niliona upo umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha ninyi kama mamlaka za kimkakati kwenye suala hili muhimu lililobeba taswira ya kitaifa ili tuweze kujadili na kushauriana kuhusu namna bora ya kulifanikisha kwa pamoja.” Alisema Bi. Makondo.

Akiielezea tume hiyo kabla ya kuelezea hatua ya maandalizi ilipofikia, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Nkasori Sarakikya alisema pamoja na kutekeleza majukumu mengine ambayo Kamisheni hii inaweza kukabidhiwa na Bunge la Wakuu wa Nchi na Serikali, tume hii pia inatekeleza majukumu makuu matatu ambayo ni ulinzi wa haki za binadamu na watu, kukuza haki za binadamu na watu na  kutoa tafsiri ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.

Akiongelea hatua iliyofikiwa, katika ziara hiyo, Mkurugenzi huyo alisema timu ya wataalam kutoka Kamisheni walikagua na kuchagua ukumbi na ofisi ambazo wanatarajia kutumia kwenye kikao cha 77 cha Kamisheni ya Haki za Binadamu na Watu. Pia, walikagua mifumo ya TEHAMA, hoteli na sehemu mbalimbali za malazi kama “self contained apartments”. Vilevile, pande zote zilifanya majadiliano juu ya Makubaliano kati ya Serikali na Kamisheni juu ya wajibu wa Serikali kama nchi mwenyeji wa Kikao cha 77 cha Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

 

Makatibu Wakuu na wawakilishi kutoka Wizara mbalimbali walipokea taarifa, wakahoji baadhi ya mambo yaliyotajwa katika taarifa na pia wakajadili changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa maandalizi katika kuhakikisha ukwamuzi kwa mambo yaliyokwama unapatikana na kushauri namna bora katika kuhakikisha mkutano huu unakiwa wa mafanikio.

Tarehe 31 Januari, 2023 Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Kamishna Remy Ngoy Lumbu (kutoka DRC Kongo) alimtembelea Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika mazungumzo na Mheshimiwa Rais, Mwenyekiti aliwasilisha ombi la Serikali ya Tanzania kuwa mwenyeji wa kikao cha 77 cha Kawaida cha Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu huku akimwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe Mgeni Rasmi katika mkutano huo. Mhe. Rais aliyakubali maombi yote mawili, na akaelekeza kwamba kikao hicho kifanyike nchini Tanzania kuanzia Oktoba, 2023 ili mahitaji yake yaweze kufanyiwa kazi wakati wa kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24.

Ridhaa ya mwitikio chanya wa Serikali ya Tanzania iliwasilishwa rasmi kwenye Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu pamoja na Umoja wa Afrika (AU) wakati wa mkutano wa Wakuu wa Nchi mwezi Februari, 2023. Kufuatia ridhaa iliyotolewa, Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliwasilisha maombi yake rasmi kwa Serikali kuandaa kikao tajwa kuanzia tarehe 20 Oktoba hadi 9 Novemba, 2023.