Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MABADILIKO YA KIUTENDAJI YAWAKUTANISHA ZAIDI YA MAWAKILI WA SERIKALI 1500

Imewekwa: 29 Apr, 2026
MABADILIKO YA KIUTENDAJI YAWAKUTANISHA ZAIDI YA MAWAKILI WA SERIKALI 1500

Zaidi ya Mawakili wa Serikali 1500 wamekutana jijini Dodoma, leo tarehe 29 Aprili, 2026 katika kikao kazi cha Mawakili wa Serikali  kilichofanyika kwa lengo la kujadili masuala ya kimkakati  yatakayoboresha utendaji kazi wao na hatimaye kuleta mabadiliko chanya kwa Taifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa kikao hicho kilichofanyika tarehe 29 Aprili, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera alisema kuwa  Serikali inawategemea Mawakili hao katika kuishauri ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi ikihusisha  mikataba  kati yake na kwenye sekta binafsi.

“Zaidi ya asilimia 70 ya malengo ya Dira 2050 yanatekelezwa na sekta binafsi,niwaombe mjielimishe kuhusu dhana ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili muweze kuishauri Serikali kuhusu masuala ya uwekezaji.”

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara Ndg. Eliakim Chacha Maswi alisema kuwa kikao kazi hiki ni kikao cha kimkakati cha kuweka upya msingi wa sekta ya sheria katika safari ya Taifa la Tanzania kuelekea DIRA 2050.

‘’Sisi ndio wasimamizi wa sekta ya Sheria  ambayo ndio msingi wa DIRA 2050, tujitambue na tuchukue hatua za kuweka mwelekeo wa tofauti wa sekta ya sheria, tuweke wazi matarajio ya wananchi na wajibu wa kila mmoja wetu ili kuhakikisha sekta hii inatimiza na kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu’’ alisema Maswi.

‘’Taifa linaweza kuwa na rasilimali nyingi sana lakini kama halina msingi na mfumo mzuri katika sekta ya sheria rasilimali hizi haziwezi kulisaidia Taifa kufikia malengo ya kiuchumi’’ aliongeza Maswi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) Wakili Ado Novemba, ameiomba Wizara ya Katiba na Sheria kuangalia namna ya kukisaidia chama hicho kutimiza majukumu yao ikiwemo  upatikanaji wa ofisi na magari kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao jambo ambalo wizara imeahidi kulitekeleza.