Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mabadiliko Yoyote ya Sheria Yatashirikisha Wadau: Dkt. Chana

Imewekwa: 30 Oct, 2023
Mabadiliko Yoyote ya Sheria Yatashirikisha Wadau: Dkt. Chana

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha wadau kwenye mabadiliko yoyote ya Sheria ili kuepuka sheria moja kubadilishwa mara kwa mara.

Dkt. Chana ametoa kauli hiyo wakati akitolea ufafanuzi ombi la Serikali la kuondoa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Shule ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania kutoka kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Sekta ya Sheria wa mwaka 2023 kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, tarehe 30 Oktoba, 2023 Jijini Dodoma.

Tarehe 18 Oktoba, 2023 Mhe. Chana aliwasilisha mbele ya Kamati hiyo Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Sekta ya Sheria wa mwaka 2023 (The Legal Sector Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2023) unaopendekeza kufanya marekebisho ya sheria ishirini na tatu (23) ambapo alitoa ombi la kuondoa katika Muswada mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania Sura ya 425.

Katika ufafanuzi wa Serikali Mhe. Waziri amezitaja sababu za kuondoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa mapendekezo ya marekebisho ya ziada kutoka Shule ya Sheria kwa Vitendo, mapendekezo ambayo hayajapitia kwenye Kamati ya Baraza la Mawaziri ya Katiba na Sheria (KB) Chombo ambacho kina wajibu kupitia Miswada yote inayowasilishwa na Serikali kabla haijawasilishwa Bungeni na sababu nyingine ni kwamba mapendekezo hayo hayajapata maoni ya umma.

Kuondolewa kwa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania Sura ya 425 kutatoa nafasi kwa Serikali kuyafanyia kazi zaidi na kisha yatawasilishwa katika Muswada mahususi kwa ajili ya kusomwa mara ya kwanza Bungeni katika Mkutano wa 13.

Akiongelea kuhusu Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachoendelea Jijini Arusha Dkt. Chana ameishukuru Kamati kuwaruhusu baadhi ya wajumbe kuhudhuria Kikao hicho ambacho kimeiweka Tanzania kwenye ramani katika usimamizi wa haki za binadamu. Aidha, ameendelea kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali Tanzania kuandaa Kikao hicho kitu ambacho kimeendelea kuiheshimisha nchi.

Katika hatua nyingine Mhe. Waziri amempongeza Mhe. Dkt. Tulia Ackson Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Akichangia katika kikao hicho Mjumbe wa Kamati Mhe. Rashid Abdallah Shangazi amesema Serikali imechukua uamuzi mzuri wa kwenda kupata maoni ya wadau. “Tunapotunga sheria hatupaswi kujifungia watu wachache, ni vema kuwashirikisha wadau mbalimbali ambao sheria hiyo inawahusu hata wakiwa wachache kiasi gani, hapa Mhe. Waziri umefanya jambo zuri la kwenda kushirikisha umma kupata mawazo yao.”

Akiahirisha kikao hicho Kaimu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Florent Kyombo amesema Kamati imeridhia sababu za Serikali kuondoa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania Sura ya 425 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge hadi mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo yatakapoletwa Bungeni baada ya Serikali kujiridhisha na maoni ya wadau.