Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Madawati ya Jinsia si kwa ajili ya wanawake pekee - Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga

Imewekwa: 17 Jun, 2023
Madawati ya Jinsia si kwa ajili ya wanawake pekee - Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga

Na William Mabusi – WKS Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Johari Musa Samizi amesema moja ya sababu za wanaume kushindwa kujitokeza kutoa malalamiko yao kwenye dawati la jinsia ni kwa kuwa hawapendi malalamiko yao kusikilizwa na mwanamke hali inayofanya kujikuta wanakosa msaada hata pale wanapouhitaji.

Bi. Samizi ameyasema hayo tarehe 12 Juni, 2023 alipokutana na kuzungumza na timu ya wataalam wa MSLAC waliofika ofisini kwake kujitambulisha ambapo pamoja na mambo mengine alipongeza jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuona wananchi wengi wa hali ya chini wanapata elimu ya sheria na kuwaagiza wananchi hususan wanaume kujitokeza kwa wingi katika kampeni hiyo kupata elimu juu ya ukatili wa kijinsia kwani wapo wanaume wanaokumbana na ukatili wa kijinsia.

Bi. Samizi amesema “kampeni hii iwasaidie watu wenye shida ya kweli, wanaume nao wapewe elimu kwani ukatili wa kijinsia ni pande zote.”

Akiwatoa hofu wanaume ya kusikilizwa na akina mama kwenye Madawati ya Kijinsia, Afande Monica Venance Sehere kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Halmashauri ya Shinyanga amesema Madawati hayo sasa yana akina baba wanaosikiliza changamoto za wanaume.

 “Kesi nyingi zinazoripotiwa ni kuhusu wanawake na watoto na hii inasababisha Dawati hilo kuonekana ni la akina mama na watoto kumbe hata wababa wanahusika isipokuwa akina baba hawaripoti malalamiko yao.” alisema Afande Monica.

Kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Masengwa Diwani wa kata hiyo Mhe. Nicodemas Simon aliwataka wananchi kutumia uelewa walioupata kwenye elimu ya sheria inayotolewa kuacha mila potofu zinaosabisha ukatili wa kijinsia na uvunjifu wa amani katika jamii na kuachana na taratibu zisizo rasmi za kumaliza kesi za unyanyasaji wa kijinsia na mimba za utotoni kwa makubaliano ya kulipishana ng’ombe kwa waliotenda vitendo hivyo kitu ambacho ni kinyume na taratibu kwani watuhumiwa hao wanatakiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa inayoongoza katika vitendo vya ukatili wa kijinsia. Mkuu wa Mkoa huo Bi. Christina Mndeme wakati anazindua kampeni hiyo mkoani kwake alisema anamatumaini makubwa kwamba kampeni hiyo itasaidia kupunguza kama siyo kumaliza kabisa vitendo hivyo.