Mama Samia Legal Aid Campaign Yapokewa kwa Kishindo Ludewa

Na Lusajo Mwakabuku & Athumani Msosole – WKS Ludewa
Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Compain - MSLAC) Mkoa wa Njombe umeambatana na zoezi la utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwenye kata na vijiji katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Njombe ikiwemo Wilaya ya Ludewa.
Akiwapokea wataalam wanaounda timu ya msaada wa kisheria kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Bi. Victoria Mwanziva alisema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imefika wakati muafaka na wananchi wa Ludewa walikuwa wanaisubiri kwa hamu kutokana na migogoro mbalimbali inayohusu masuala ya kisheria inayowakumba wananchi wake.
“Sisi wana Ludewa tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Kampeni hii ya Kitaifa, Wataalam wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria wapo Ludewa na sisi Wilaya ya Ludewa tumeipokea kampeni hii kwa mikono miwili na kazi inaendelea wilayani hapa” Alisema DC Mwanziva.
Aidha mara baada ya timu kuwasili wilayani na kujitambulisha katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, timu ya wataalam wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Bi. Manziva walielekea katika kituo cha Radio kilichopo Ludewa mjini (Rafiki FM) na kuelezea kuhusu ujio wa Mama Samia Legal Aid Campaign wilayani humo kabla ya kuendelea kutoa Elimu mashuleni na mikutano wa hadhara kwa lengo la kuelimisha jamii na kusikiliza changamoto mbalimbali za Kisheria na kuzipatia ufumbuzi.
“Ludewa tumeibeba hii kampeni na tunaenda bega kwa bega na team iliyopo hapa, tunawashukuru sana kwani kampeni hii itatoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi pamoja na kufanya uwakilishi kwa wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili na mahakamani lakini pia kupitia kampeni hii, Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata, Watendaji wa Vijiji na Kata watajengewa uwezo na hivyo kuimarisha upatikanaji wa haki”. Aliongeza Bi. Mwanziva.