Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MASWI AWAONYA MADEREVA WAJIEPUSHE NA UZEMBE, AWATAKA WAJITAFAKARI

Imewekwa: 03 Jun, 2025
MASWI AWAONYA MADEREVA WAJIEPUSHE NA UZEMBE, AWATAKA WAJITAFAKARI

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Chacha Maswi amewaagiza madereva wizarani hapo wajitafakari na waendeshe magari kwa umakini mkubwa huku akiwaagiza pia kuzingatia maadili ya kazi yao na kuwaonya wajiepushe na uzembe.

Maswi ameyasema hayo mapema  June 2, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa wizarani hapo alipokua akizungumza na madereva wa wizara hiyo huku akiagiza pia kufanyika kwa tathmini ya kuwapima madereva hao.

“Dereva anayekimbia sana anawahi wapi na ili iweje, lakini pia tuna madereva waandamizi hapa nawataka mshauriane, muelekezane na muonyane ili wote muwe sawa, msioneane aibu wala kuogopana kama unaona mwenzako anaenda isivyo unamshauri”, amesisitiza Maswi.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt Franklin Rwezimula amewaasa madereva hao kuyajali na kuyatendea haki magari kwani ndio ofisi zao hivyo wajitahidi kuyahudumia kwa usafi na kufanya matengenzo kwa wakati.

“Gari ndio ofisi ya dereva, unapaswa kulipenda na kulithamini, lifanyie usafi na service kwa wakati, dereva usipokuwa na gari au gari lako likiwa na hali mbaya unakua huna kazi”, ameongeza Dkt Rwezimula.

Kwa upande wake Dereva Mwandamizi Otmar Haule kwa niaba ya madereva wenzake amemshukuru Katibu Mkuu pamoja na viongozi alioambatana nao ambao ni Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Mkurugenzi Msaidizi wa utawala na Afisa Usafirishaji.

“Ningependa kuwashukuru viongozi wetu kwa ushauri mzuri wa kutujenga na kutusaidia kuboresha utendaji wa kazi zetu, tuna ahidi tutashauriana, tutaonyana na kubadilishana uzoefu baina yeti ili sote tufanye kazi kwa kufuata maadili na taratibu zinazotakiwa”, amesema Haule.