Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mawakili wa Serikali Tuishauri Ipasavyo Serikali

Imewekwa: 20 May, 2024
Mawakili wa Serikali Tuishauri Ipasavyo Serikali

Hyasinta Kissima-WKS Arusha

Naibu Waziri  wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amewataka Mawakili wa Serikali kuishauri ipasavyo Serikali na Taasisi zake wakiwemo Viongozi kuhusu namna ya kushughulikia na kumaliza migogoro na Wananchi au Wawekezaji bila kuathiri maslahi ya Nchi.

Mhe. Sagini ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yanayofanyika kwa muda wa siku tatu  kuanzia Mei 20, 2024, Lush Hotel Jijini Arusha.

"Kwenye eneo hili napenda  kuwashauri kuwa more 'proactive rather than reactive' mtakapoona Viongozi wetu katika utendaji wao kuna dalili ya kuleta migogoro kwenye utekelezaji wa mikataba, msisubiri mambo yaharibike. Ninyi Mawakili wa Serikali mpo, mkisubiri yakaharibika watu wakaenda kwenye vyombo vya kutoa haki kama Mahakama au  Mabaraza ya Usuluhishi ya  ndani na nje ya nchi maana yake kazi imeanza kuwa ngumu. Lakini kama tungewahi tukatoa ushauri mapema tungezuia hali isiwe mbaya." Alisema Naibu Waziri Sagini

Aidha, ameipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa  mafanikio makubwa ikiwemo kuitetea Serikali katika mashauri ya madai na usuluhishi jambo ambalo limepelekea kuokoa fedha nyingi za Serikali katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwa ofisi.

Aliendelea kusema, matumaini ya Wizara ya Katiba na Sheria  ni Mawakili hao kuendelea kuyatumia mafunzo hayo kama  chachu katika kuendeleza mafanikio hayo  na kuwafanya kutoridhika bali kuamsha ari mpya katika kuyaishi na kuyaendeleza kwa faida ya Serikali, Nchi na Wanachi.

Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende aliainisha ajenda kuu tatu katika mafunzo hayo ambapo ajenda ya kwanza ikiwa ni uzinduzi wa nembo ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo itatumika kama utambulisho katika mawasiliano mbalimbali, ajenda ya pili  ikihusisha mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yanayohusu uwasilishaji wa mada mbalimbali na majadiliano na ajenda ya tatu ikiwa ni  kufanya tathmini ya namna ambavyo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Serikali zimefanikisha kuendesha na  kuratibu uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi nje na ndani ya nchi.

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali tangu mwaka 2020 imekuwa na utaratibu wa kuandaa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali ili kuongeza maarifa  na ujuzi zaidi katika maeneo mtambuka ambayo Mawakili hujishughulisha nayo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa weledi mkubwa ambapo kwa mwaka 2024, jumla ya Mawakili 500 kutoka Wizara zote Nchini,Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar, Taasisi za Umma, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Taifa, Wakala wa Serikali, Mashirika ya Umma, Mamlaka za Udhibiti na Vyuo mbalimbali hapa Nchini wameshiriki.