WANANCHI ZAIDI YA 400,000 WANUFAIKA NA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA PWANI
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bw. Richard Kayombo, amesema usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala una mchango mkubwa katika kudumisha amani, kuimarisha mshikamano na kuchochea maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.
Kayombo ameyasema hayo wakati akiahirisha zoezi la siku 10 la utoaji wa Huduma za Msaada wa Kisheria mkoani Pwani kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili, huku akisisitiza Sekretarieti ya utekelezaji wa kampeni hiyo kuendelea kulifanyia kazi suala la usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani, Bi. Grace Tete, amesema kuwa wanawake wamejitokeza kwa wingi zaidi kupata huduma hizo ikilinganishwa na makundi mengine, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kusogeza huduma za msaada wa kisheria karibu na wananchi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Pwani, Mratibu wa kampeni ambaye pia ni Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Innocent Magesa, amesema zaidi ya wananchi 400,000 wamefikiwa na kunufaika moja kwa moja na huduma za msaada wa kisheria.
Aidha, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Osborn Paissi, amesema kampeni hiyo imefanikiwa kuwafikia wafungwa na mahabusu 504 katika magereza 7 na vituo 8 vya polisi mkoani Pwani, kwa kuwapatia huduma za msaada wa kisheria zinazolenga kuwawezesha kuelewa haki zao na taratibu za kisheria.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili inalenga kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi, kuongeza uelewa wa sheria na kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi wa makundi mbalimbali, wakiwemo wale walio katika mazingira magumu.