MSLAC AWAMU YA PILI KUJA KIDIJITALI
Katika kuelekea kuanza kwa awamu pili ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani Shinyanga mnamo tarehe 6 Mei, 2026, Wizara ya Katiba na Sheria imetoa mafunzo ya matumizi ya TEHAMA kwa wataalamu wakati wa utoaji wa huduma kwa Wananchi ili kuhakikisha uratibu, ufuatiliaji na uwekaji kumbukumbu unaofaa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Dkt. Nuru Yunge amesema kuwa kupitia Kampeni hii changamoto mbalimbali za wananchi zinatarajiwa kupatiwa ufumbuzi ikihusisha migogoro ya muda mrefu ambayo wananchi wamekuwa wakiiripoti kwa viongozi mara kwa mara.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Ufuatiliaji na Uzingatiaji Msaada wa Kisheria kutoka wizarani Bw. Osborn Paiss, amesema kuwa awamu ya pili ya utekelezaji wa Kampeni umeambatana na maboresho mbalimbali ikihusisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utekelezaji wa Kampeni.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Halmashauri nne za mkoa huo ambazo ni ; Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Manispaa ya Shinyanga, Manispaa ya Kahama na Halmashauri ya Ushetu, na kuendelea tarehe 5 Mei 2026 katika Halmashauri ya Msalala na Kishapu.
Awamu ya pili ya Kampeni hii itaanza rasmi tarehe 6 Mei, 2026 hadi tarehe 20 Mei, 2026 ambapo itafanyika katika Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga.