MSLAC Itumike Kutafuta Suluhu na Sio Mshindi

Na Hyasinta Kissima – WKS Njombe
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko amewataka watoa huduma za Msaada wa Kisheria kuitumia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika kufanya utatuzi wa migogoro badala ya kutafuta mshindi miongoni mwa jamii.
Dkt. Biteko aliyasema hayo Mei 26, 2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) Mkoani Njombe iliyofanyika katika Halmashauri ya Mji ya Njombe.
Dkt. Biteko amesema kuwa, ni vyema Wananchi kuacha misimamo iliyopitiliza wakati timu ya Mawakili itakapokuwa inawasikiliza na badala yake wasimamie kwenye ukweli.
“Maandiko yanasema ukijua kweli itakuweka huru nawe utakuwa huru kweli kweli na mawakili simamieni ukweli mtapokuwa mnasikiliza watu hawa watakaokuja kwenu,” alisema Dkt. Biteko.
Aliendelea kusema, “Migogoro iliyopo ya jamii miongoni mwenu iweze kuisha bila ya kusababisha madhara makubwa, ukiona mahali fulani mtu amenyanyua upanga akamuumiza mtu mwingine, ukiona mahali fulani mtu ameamua kumuua mtu mwingine ujue kuna shida. Ukiona mahali fulani mtu ameamua kumfanyia ukatili mtu mwingine au mahali fulani mtu ameamua kumnyanyasa mtu mwingine ni kwa sababu kuna mazingira ya kutokutambua wajibu wa kila mmoja miongozi mwa jamii.” Alisema Dkt. Biteko.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Kamati ya Tume ya Haki Jinai ambayo lengo lake lilikuwa ni kuboresha mfumo wa upatikanaji wa haki kwa umma.
“Tume ile ilikuja na mapendekezo iliona mambo mengi ndani ya jamii na migogoro mingi ambayo ipo kwenye jamii, miongoni mwa migogoro hiyo ni migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, na utawala bora maana yake sisi viongozi tumekuwa sehemu ya migogoro hiyo,” alisema Dk. Biteko.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Pindi Chana alisema tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia jumla ya mikoa saba imefikiwa.
Dkt. Chana aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Ruvuma, Shinyanga, Singida, Simiyu, Manyara, Dodoma na sasa mkoa wa Njombe.
Alisema katika mikoa sita migogoro 5,16 imetatuliwa kati ya 4,942 na kufikia wananchi 4,15,000.
Aliwataka wananchi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi ili kupata fursa ya msaada wa kisheri kupitia kampeni hiyo itakayofanyika kwa muda wa siku 10.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amesema kuwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Wananchi wenye matatizo mbalimbali ya Kisheria wamefikiwa na kupatiwa huduma za msaada wa kisheria bure na kutatua changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.