Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MSLAC Kutoa Elimu Mkesha wa Mwenge – DC Makete

Imewekwa: 30 May, 2024
MSLAC Kutoa Elimu Mkesha wa Mwenge – DC Makete

Na William Mabusi – WKS Makete

Mkuu wa Wilaya ya Makete Bw. Juma Sweda amefurahishwa na utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayoendelea kutekelezwa Wilayani humo na kuwasilisha ombi kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ili timu hiyo irudi kutoa elimu siku ya mkesha wa Mwenge utakaofanyika tarehe 18 Juni, 2024 Kata ya Mfumbi.

Mkuu huyo wa Wilaya ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Masisiwe Kata ya Ukwama Mei 29, 2024 alipokwenda kujionea utekelezaji wa Kampeni hiyo.

“Mie mwenyewe nimesikiliza elimu inavyotolewa nikasema ewaaa! Nimefurahishwa na ufundishaji wa Vijana hawa kutoka kwa Waziri Dkt. Pindi Chana dada yetu anayetoka Ludewa, ambaye naye aliagizwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuja kutoa elimu ya sheria, kusikiliza kero zenu  na kuwashauri. Elimu wanayoitoa naamini itasaidia kuwapata kutoka miongoni mwenu washauri watakao msaidia Mwenyekiti wenu wa kijiji kutatatua migogoro,” alisema na kuongeza;

”Elimu hii itufungue macho kujua je kuna haja ya kuendelea na mgogoro uliokuwepo kati ya mume na mke, jirani na jirani. Na wakati mwingine unajua mgogoro unaweza kuwa ni hatua moja tu inagombewa kwenye mpaka. Tarehe 18 Juni, 2024 utafanyika mkesha wa Mwenge Kata ya Mfumbi, nimeongea na dada yetu Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana kuiomba timu hii na yeye mwenyewe wawepo kutoa elimu kwa wananchi watakaokuwepo siku hiyo.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya Makete Bw. William Makufwe ambaye pia alitembelea timu hiyo amewataka wananchi kuitumia vizuri Kampeni hiyo kwani imekuja ili wananchi wapate haki yao iliyopotea au kuchelewesha.

Akijibu swali la Bw. Alfred Masharubu Pira mkazi wa kijiji cha Masisiwe aliyetaka kujua kama kumpendelea mtoto mmoja kwenye wosia  ni sawa kisheria, Mwanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Fredrick Makamba amesema hakuna shida ilimradi zipo sababu za kufanya hivyo.

“Faida ya kuandika wosia pamoja na mambo mengine ni kuelekeza mali yako igawanywe vipi utakapofariki. Aidha, katika kuandika wosia unaruhusiwa kumnyima mwanao wa kumzaa kurithi mali endapo utakuwa na sababu za kufanya hivyo. Sababu hizo ni pamoja  na kama itagundulika mwanao ameshiriki tendo la ndoa na mama yake, kutapanya mali, hakuhangaika kukuuguza wakati wa ugonjwa.” Alisema Bw. Makamba.