Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MSLAC Yatatua Mgogoro wa Familia Uliodumu Miaka Mitatu

Imewekwa: 14 Jan, 2024
MSLAC Yatatua Mgogoro wa Familia Uliodumu Miaka Mitatu

Na William Mabusi – WKS Singida

Kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) inayoendelea kutekelezwa mkoani Singida imeamua ugomvi na kuunganisha familia ya watoto saba ya Bw. Temistocules Kokula na Bi. Neema Joseph wa kijiji cha Mwisi Kata ya Lighwa Halmashauri ya Ikungi. Ugovi wa muda mrefu uliokuwa unapelekea vipigo kwa Bi. Neema na watoto ulimfanya aondoke kurudi kwao mwaka 2021 na kuwaacha watoto ambao wamekuwa wakimtoroka baba yao na kumfuata kutokana na malezi ya baba ambayo yamekuwa ya vipigo vya mara kwa mara.

Mgogoro huo uliibuka baada ya Bw. Kokula kufika kwenye timu ya MSLAC akilalamika kuwa watoto wake wamemtoroka na kurudi kwa mama yao. Ili kujua undani wa mgogoro huo, timu ya MSLAC chini ya Mratibu wake Wilayani humo Bw. Laurent Burilo iliwaita wanandoa hao kwenye kikao.

Haikuwa kazi rahisi kumshauri Bi. Neema kurudi kwa mumewe ili kuwalea watoto, hata hivyo baada ya wote wawili kupewa elimu sheria na madhara ya ukatili wa kijinsia na timu ya MSLAC ambayo pamoja na wataalam wengine lakini pia inaambatana na Afisa Ustawi wa Jamii, Afisa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto walielewa na Bw. Kokula kukiri kuwa wataenda kuishi kwa amani.

Akihitimisha mgogoro huo Afisa wa Dawati la Polisi la Jinsia na Watoto Bi. Dalahile Mahende kutoka Halmashauri ya Ikungi amesema  Ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Ikungi wataendelea kufuatilia mwenendo wa familia hiyo na endapo ikibainika kuendelea kwa vitendo hivyo, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa.