Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

NDUMBARO ATAJA “REFORMS” 15 ZILIZOFANYWA NA UONGOZI WA RAIS SAMIA

Imewekwa: 09 Jun, 2025
NDUMBARO ATAJA “REFORMS” 15 ZILIZOFANYWA NA UONGOZI WA RAIS SAMIA

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro ametaja mabadiliko 15 ya sheria ya Uchaguzi yaliyofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuimarisha demokrasia na utawala bora nchini. 

Akizungumza leo juni 9 2025 mjini Tarime Mkoani Mara alipokuwa akifungua mafunzo ya elimu ya Kisheria kwa viongozi wa kata, Dkt. Ndumbaro amesema mabadiliko hayo yanadhihirisha dhamira ya kweli ya Rais Samia ya kujenga mfumo huru, wazi na wa haki wa uchaguzi.

Amesema mabadiliko hayo yamejumuisha kufutwa kwa sheria ya zamani ya uchaguzi ya taifa na ile ya serikali za mitaa, na badala yake kutungwa sheria mpya ya uchaguzi inayoendana na matakwa ya sasa ya kidemokrasia.

"Kwa mara ya kwanza, Tanzania imepata sheria mahsusi ya Tume Huru ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024, hatua inayolenga kuimarisha uhuru na uwajibikaji wa taasisi hiyo muhimu, mabadiliko hayo pia yamefuta nafasi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kuwa msimamizi wa uchaguzi ambapo sasa wasimamizi watapaswa kuomba nafasi hizo na kufanyiwa usaili na Tume Huru", amefafanua Dkt Ndumbaro.

Ameongeza kuwa majina ya wasimamizi wa uchaguzi kwasasa yatatangazwa kupitia Gazeti la Serikali na kubandikwa hadharani, huku wale waliowahi kuwa viongozi wa kisiasa ndani ya miaka mitano hawataruhusiwa kushika nafasi hizo. 

Dkt Ndumbaro amefafanua kuwa mabadiliko hayo pia yamewezesha Wananchi, vyama vya siasa na wadau wengine kuwa na haki ya kuweka pingamizi dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi ili kuongeza uaminifu wa umma katika mchakato wa uchaguzi na kuondoa mianya ya upendeleo au migongano ya maslahi.

Aidha mabadiliko mengine yamewezesha kuruhusu wafungwa na mahabusu ambao vifungo vyao havizidi miezi sita kujiandikisha na kushiriki katika upigaji kura na ili kuwezesha hilo, vituo maalum vya kupigia kura vitaanzishwa ndani ya magereza. 

Dkt Ndumbaro ameeleza kuwa uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi utafanyika kwa uwazi na kuzingatia sifa, ili kuhakikisha tume hiyo inaendeshwa na watu wenye uadilifu na weledi.