Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Rais Samia Afungua Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Jumuiya ya Madola

Imewekwa: 04 Mar, 2024
Rais Samia Afungua Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Jumuiya ya Madola

Na William Mabusi – WKS Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua Mkutano wa siku tano wa Mawaziri wa Sheria kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo huku akisisitiza matumizi ya teknolojia ya kidijitali kuharakisha upatikanaji haki.

Ufunguzi wa mkutano huo wenye nchi wanachama hamsini na sita umefanyika leo tarehe 04 Machi, 2024 katika Hotel ya Golden Tulip Visiwani Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

“Nashukuru Jumuiya ya Madola kwa kuchagua nchi yetu Tanzania na hasa hapa Zanzibar kufanyia mkutano huu mkubwa ambao unalenga kujadili pamoja na mambo mengine jinsi maendeleo ya kidijitali yanavyowezesha uboreshaji wa upatikanaji  wa haki kwa watu.” Alisema.

Mhe. Rais amesema teknolojia za kidijitali zikiundwa na mifumo iliyorahisishwa zinamsaada mkubwa katika kutoa njia bunifu na rahisi kwa watu kuweza kupata suluhu kupitia mifumo rasmi na isiyo rasmi ya utoaji haki.

Akielezea mikakati mbalimbali inayofanywa na Serikali katika kusimamia utoaji haki amesema “Serikali ilizindua kampeni kubwa inayoitwa Mama Samia Legal Aid Campaign kushughulikia utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria, upatikanaji wa haki kwa wananchi katika ngazi zote, kushughulikia masuala mtambuka yanayohusu haki za binadamu na watu, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya wanawake na watoto, masuala ya usimamizi wa ardhi, mirathi na utatuzi wa migogoro."

Awali akitoa hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema chini ya utawala wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa katika masuala ya uzingatiaji amani, demokrasia na maendeleo.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola MH. Patricia Scotland KC Akitoa salaam katika mkutano huo ametoa pole kwa Tanzania kwa kuondokewa na Rais wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi. “Katika mkutano huu tunaungana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzani katika kipindi hiki cha maombolezo ya Kitaifa  kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya Pili, tupo hapa Zanzibar ambapo Marehemu Rais alikuwa mwanafunzi, mwalimu na kiongozi. Tunasikitika zaidi kwani Rais Mwinyi alikuwa ni kiongozi wa Serikali aliyeleta mageuzi katika teknolojia kwa kuruhusu matumizi ya simu za mkononi na kompyuta na leo tunakusanyika chini ya kaulimbiu ya teknolojia na uvumbuzi inavyoweza kutumika ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati kwa raia."

Mkutano huo wa Mawaziri wa Sheria kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola unafanyika nchini kwa mara ya kwanza, utahitimishwa tarehe 8 Machi, 2024 ambapo Mgeni Rasmi siku hiyo anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.