Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

SEMA NA WAZIRI HAICHAGUI KERO

Imewekwa: 22 Apr, 2026
SEMA NA WAZIRI HAICHAGUI KERO

Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kikamilifu kushughulikia malalamiko yote ya wananchi yanayowasilishwa kupitia programu ya Sema na Waziri katika Kituo cha Huduma kwa Mteja, kwa weledi, ufanisi na uwajibikaji.

Akizungumza Aprili 22, 2026, Mtumba jijini Dodoma wakati wa programu hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Homera amesisitiza kuwa Wizara ina wataalamu wa kutosha, wenye ujuzi na ari ya kufanya kazi, ambao wako tayari kushughulikia changamoto za Watanzania popote walipo nchini.

Mhe. Homera ameeleza kuwa programu ya Sema na Waziri ni endelevu, ambapo wananchi wataendelea kupata fursa ya kuwasilisha malalamiko yao mara mbili kwa mwezi ambapo pia wizara itahakikisha inatoa mrejesho wa kina kuhusu migogoro na changamoto zote zinazowasilishwa, ili kuongeza imani ya wananchi kwa huduma za serikali.

“Hatuchagui kero, tunapokea kero zote, tunasikiliza changamoto zote, na tunaendelea kuzifanyia kazi kwa bidii,” amesema Mhe. Homera

Ameongeza kuwa Wizara imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan walioko maeneo ya pembezoni, ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kuwasilisha changamoto za kisheria zinazowakabili maoni na ushauri, kwa lengo la kuboresha huduma na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.

Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kutoa huduma za kisheria kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Wizara. Mwananchi yeyote mwenye changamoto za kisheria, ushauri ama maoni anaweza kupiga simu bure kwa namba 0262 160 360 au 0800 004 004 ama kutuma ujumbe kwa njia ya WhatsApp kwa namba 0739 101 910, Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 01:30 Asubuhi  hadi saa 11:30 jioni.