Serikali Ina Dhamira Thabiti ya Kuwalinda Watoto Dhidi ya Ukatili

Na Lusajo Mwakabuku – WyKS Dar es salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula ameongoza matembezi ya amani na kushuhudia utolewaji wa Msaada wa Kisheria dhidi ya vitendo vya ukatili na mauaji kwa watoto, hafla iliyoandaliwa na Tanganyika Law Society (TLS) akimwakilisha Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bwana Eliakim Maswi.
Katika hafla hiyo iliyofanyika tarehe 18/10/2024 Naibu Katibu Mkuu amemesema Tanzania ni moja ya nchi zenye Mfumo wa Kisheria thabiti inayowalinda Watoto dhidi ya vitendo vya ukatili. Hata hivyo, kutokana na kukua kwa maendeleo ya kiteknolojia, vitendo vya ukatili dhidi ya Watoto vimekuwa vikiibuka katika namna tofauti tofauti. Jambo hili, limepelekea Serikali kwa kushirikiana na wadau, kuendelea kuchukua hatua na mbinu mbalimbali katika kukabiliana navyo.
Akivitaja baadhi ya vifungu vya sheria vinavyomlinda mtoto, Naibu Katibu Mkuu alisema Sheria ya Mtoto Sura ya 13, inatoa mfumo mpana wa haki na ulinzi wa Watoto dhidi ya unyanyasaji na unyonyaji. Akaongeza kuwa Sheria inawapa jukumu wazazi na jamii kwa ujumla kusimamia na kulinda haki za Watoto ikiwemo haki ya kupata elimu, afya, malazi, chakula, malazi na kuwalinda dhidi ya vitendo vya kijinai kwa mujibu wa Sheria za nchi.
“Ulinzi wa mtoto umeanzia kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, kwani imeweka mifumo ya kisheria wa ulinzi wa haki za watoto. Kupitia, Ibara ya 14 inatambua haki ya kuishi, wakati Ibara ya 13 inahakikisha usawa mbele ya Sheria na ulinzi dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote. Masharti haya ni muhimu kwani yanaweka msingi wa kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na ubaguzi,” alisema Dr. Rwezimula.
Akitoa salamu za awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Wakili Bonifasi K. Mwabukusi – rais wa TLS aliwataka watanzania wote kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili waweze kuchagua viongozi wanaodhani wanafaa na watakaoweza kulinda haki za watoto.
Kutokujiandikisha kupiga kura ni ukatili kwa Watoto, kutojiandikisha kunatoa fursa ya kupata viongozi wasio bora ambao watashindwa kulinda haki za Watoto. Hivyo hata nyie Mawakili msipojiandikisha maana yake mnakuwa mawakala wa ukatili huu. Jitokezeni kujiandikisha na pia wote tupige kura”. Alisema Mwabukusi.
Aidha Mwabukusi akatumia nafasi hiyo kuipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwa Wizara haijawajengea ukuta bali imekuwa “Proactive” huku akihimiza Wizara taasisi nyingine ziige mfano wa MoCLA na kutoiogopa TLS kwani Kazi ya TLS ni kuhakikisha utawala bora na si vinginevyo.
Akisoma risala ya Mawakili wanawake wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Wakili Laetitia Petro Ntagazwa ambaye ni Makamu wa rais wa TLS na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi alisema wanashukuru kwa kiasi kikubwa kwani Serikali imeendelea kuonesha ushirikiano mzuri hasa mara baada ya uongozi mpya wa TLS kuingia madarakani na wakaomba Serikali iweze kuwatengea bajeti katika utekelezaji wa majukumu yao. Pia wakaishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana nao kupitia Mradi wa Mama Samia Legal Aid Kampeni na wakaahidi kuendelea kushirikiana vema kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.