Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Serikali itaendelea kulinda na kukuza upatikanaji haki – Dkt. Chana

Imewekwa: 10 Jan, 2024
Serikali itaendelea kulinda na kukuza upatikanaji haki – Dkt. Chana

Na William Mabusi – WKS Singida

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali itaendelea kulinda na kukuza upatikanaji haki nchini kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya kisera ya Kitaifa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha  kunakuwa na usawa  mbele ya sheria, wananchi  wanalindwa na wanapata  haki kupitia vyombo vya haki.

Dkt. Chana ameyasema hayo Mkoani Singida alipokuwa anazindua utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ijulikanayo kama Mama Samia Legal Aid Campaign iliyoanza kutekelezwa mkoani humo leo tarehe 10 Januari, 2024.

“Lengo la utekelezaji wa kampeni hii ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini ambayo ni utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania  ibara ya 8 (1)  (b) na Ibara ya 13 (1) zinazoweka msingi wa haki na usawa na ustawi wa wananchi.”

Ameyataja mafaniko makubwa yaliyopatikana tangu kuanza kutekelezwa kwa kampeni hiyo mwezi Aprili 2023 hadi kufikia Oktoba, 2023 ambapo jumla ya mikoa mitano imeshatembelewa, kuwa  ni pamoja na jumla ya  migogoro 6,365 iliyohusu  masuala ya ardhi, ndoa, mirathi na matunzo ya watoto ilipokelewa ambapo  kati ya hiyo migogoro  488 ilitatuliwa na kuhitimishwa. Migogoro 5,877 inaendelea kushughulikiwa katika mamlaka  mbalimbali za kimahakama na kiutawala na Wizara kupitia Waratibu na Wasajili wa mikoa na wilaya imeendelea kufuatilia utekelezaji wake.

Aidha, wananchi 2,055 (Wanaume1,035 Wanawake 1,020) walisajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kupitia Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu – RITA, kumekuwepo na ongezeko la   uelewa na uwajibikaji wa Watendaji wa Vijiji, Kata,  Halmashauri, Viongozi wa kidini na kimila, Wanafunzi na Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika kuwahudumia wananchi na kuwasaidia kudai na kupata haki zao baada ya kujengewa uwezo katika masuala mbalimbali ya sheria, haki za binadamu na utawala bora.

Kampeni ya  Msaada wa Kisheria inatokana na adhma ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kwamba  kila mwananchi anafahamu masuala ya kisheria ikiwemo haki na wajibu wake na kwamba kila mwananchi anaifikia haki na wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili waweze kufikia haki kupitia huduma za msaada wa kisheria.

Kupitia kampeni hiyo, msaada wa kisheria unatolewa bure katika Halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida hadi tarehe 19 Januari, 2024, lengo likiwa ni kufikia jumla ya Kata 70 na vijiji 210.  Hivyo wananchi wote  wa Mkoa wa Singida kwenye kata ambazo kampeni hiyo itafanyika wameombwa kuitumia fursa hiyo kwa kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu  kwa kupata elimu na huduma mbalimbali za masuala ya kisheria  zitakazotolewa. Aidha, amewasihi viongozi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalam wanaotekeleza kampeni.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Singida Bw. Peter Serukamba amesema mkoa ulianza maandalizi ya kuipokea kampeni tangu ilipozinduliwa mwezi Aprili 2023 Jijini Dodoma. Ameongeza kuwa kila Halmashauri ina watoa huduma ambao wamepata mafunzo ya kutekeleza kampeni hiyo hivyo wataitumia fursa hiyo ipasavyo kwa mustakabali wa kuendeleza amani ya mkoa na kumaliza migogoro inayochelewesha shughuli za maendeleo.