SERIKALI ITAKAMILISHA UJENZI NA UKARABATI WA MAJENGO YA MAHAKAMA 2025/2026

Naibu Waziri Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini, amesema kuwa utekelezaji wa mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya mahakama unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2025/2026..
Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kalenga Bungeni jijini Dodoma Jana Juni 11, 2025,lililouliza lini serikali itaanza ujenzi wa mahakama ya tarafa ya Kiponzeli Kalenga, Mhe. Sagini alisema kuwa majengo ya mahakama yanajengwa na kukarabatiwa kwa awamu kadri fedha zinavyopatikana.
“Mahakama ya Tanzania imeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na kukarabati majengo ya mahakama wa mwaka 2021/2022 /2026 ambapo kwa Sasa hatua za kuhuisha mpango huo kinaendelea ili kuhakikisha utekelezaji unakamilika katika kipindi Cha 2025/2026” alisema Mhe. Sagini.
Aidha Mhe. Sagini amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa kata ya Kiponzeli kwa kushirikiana na Mahakama na kuanza kufanya ukarabati katika jengo la Sasa la mahakama hiyo.
Akijibu swali la Mhe. Zakaria Issa , Mbunge wa Jimbo la Mbulu aliyetaka kufahamu ni lini ujenzi wa mahakama ya wilaya ya Mbulu uliosimama kwa muda utaendelea, Mhe Sagini alisema kuwa Serikali kupitia Idara ya Mahakama hususani Mtendaji Mkuu wa Mahakama itahakikisha kwamba mpango uliopitishwa unaendelea na ujenzi wa mahakama ya Mbulu unakamilika kama ilivyopangwa.