Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Shinyanga yaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign.

Imewekwa: 11 Jun, 2023
Shinyanga yaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign.

Na Lusajo Mwakabuku & William Mabusi – WKS Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ameiahidi Wizara ya Katiba na Sheria na wadau inaoshirikiana nao katika kuendesha kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria - Mama Samia Legal Aid Campaign kutoa ushirikiano wa hali na mali katika kufikia malengo ya kampeni hii ya kutoa msaada wa kisheria kwa watanzania wote hasa wale waishio maeneo ya pembezoni huku akiagiza kata zote zihakikishe zinanatenga maeneo maalum ambayo watoa huduma wataweza kuongea na mwananchi mmoja mmoja kwa faragha.

Mheshimiwa Mndeme alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia kabla ya kuzindua rasmi utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Shinyanga hafla iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba Shinyanga mjini leo tarehe 11/06/2023 huku akiwaalika wakazi wote wa mkoa wa Shinyanga kushiriki Mama Samia Legal Aid Campaign itakayotolewa bure kwa wanachi katika Halmashauri zote sita kuanzia tarehe 11 - 21 Juni, 2023.

“Kwa mara nyingine tena, ninatoa wito kwamba sisi sote tushikamane katika kumuunga mkono Kiongozi wetu, Mama yetu, Mlezi wetu na Mtetezi wa Wananchi hususan wanyonge Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika kuondoa kadhia na viashiria vyote vya kuminya upatikanaji wa haki hususan ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto ambayo ndiyo changamoto kubwa ya Mkoa wa Shinyanga”. Alisema Mhe. Mndeme

Mkuu wa Mkoa huyo aliongeza kuwa kampeni hii inatukumbusha watanzania wote uwajibikaji na usimamizi wa maamuzi yenye kuleta haki na akatumia fursa hiyo kuwambusha watumishi wote kutojihusisha na masuala ya rushwa inayopelekea kuzorotesha upatikanaji haki. Aidha Mhe. Mndeme alimuahidi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa katika utekelezwaji wa Kampeni hii kwa kipindi cha miaka mitatu, ofisi yake itasimamia maadili kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa haki kwa usawa.

Akitoa salaam na kumkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema Wizara itaendelea kushirikiana na Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kuhakikisha Kampeni hiyo inatekelezwa ipasavyo ili kuwafikia watanzania kwenye Kata na Mitaa yote nchini.

Mhe. Gekul amesema Wizara ya Katiba na Sheria inamshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kudumisha utawala wa sheria; uzingatiwaji wa haki za binadamu na watu na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote lakini kwa jicho la kipekee kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.

“Huduma ya msaada wa kisheria kuwafikia wananchi bure ni mapenzi na upendo mkubwa wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mwananchi wa hali ya chini,” alisema Mhe. Gekul.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu Mama Samia Legal Aid Campaign, Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo ametaja mafanikio ya kampeni hii toka ilipozinduliwa Mkoani Dodoma na kuendelea katika mkoa wa Manyara kuwa ni pamoja na kusuluhishwa kwa migogoro mingi ya kijamii na hata kifamilia iliyohusu ardhi iliyodumu miaka minne, mitano, na mwingine miaka kumi kulikopelekea watu hawa ambao walikuwa hawasalimiani na hata hawazikani kumaliza tofauti zao.

“Ziko familia ambazo wanafamilia walikuwa hawaongei kutokana na migogoro inayohusiana na ardhi, mirathi na sasa wamesuluhishwa katika Kampeni na wameungana katika kujenga familia zao na taifa kwa ujumla.” alisema Bi. Makondo.

Aidha Bi. Makondo amesema kwa kuwa kuna uwezekano mazingira ya mikoa hiyo kuwa sawa na Shinyanga hivyo uzoefu wa utatuzi wa migogoro hiyo utasaidia Kampeni hiyo kushughulikia masuala yote ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi na wosia na kuelimisha jamii kuhusu haki na wajibu wao wa kisheria na kikatiba kwa mbinu na uzoefu uliopatikana mikoa iliyotangulia na hivyo kuwezesha kampeni hiyo kufanyika kwa mafanikio makubwa zaidi katika mkoa wa Shinyanga.

Umuhimu wa kampeni hii ni wa kipekee katika kuongeza wigo wa ufikiwaji haki kwa wananchi, hususan walio vijijini na  ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili. Kampeni hii pia imekuwa msingi mzuri wa kujenga uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria; jambo ambalo ni muhimu katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini. Hii ni kampeni ya miaka mitatu yenye lengo la kufikia mikoa yote nchini huku ikitarajiwa kuhitimishwa mwaka 2026.