Simamieni Malalamiko ya Ukiukwaji wa Haki za Binadamu - Dkt. Mwandambo

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Dkt. Stephen Mwandambo amewataka Watendaji wa Kata kusimamia malalamiko ya wananchi ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu.
Dkt. Mwandambo ameyasema hayo tarehe 15 Machi, 2025 wakati akifungua mafunzo ya Uraia na Utawala Bora kwa Kamati ya Usalama Wilaya, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Watendaji wa Kata wa Halmashauri ya Jiji la Tanga.
“Mafunzo haya yatamsaidia Mkurugenzi kutoa nafuu kwenye utekelezaji wa majukumu na tunategemea kuona huduma zimeboreshwa katika ngazi zote baada ya mafunzo haya.“
Mwandambo amesema kupitia mafunzo waliyopata watatekeleza kwa vitendo na kuhakikisha falsafa ya “4R“ ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inasambaa kutoka katika ngazi za chini mpaka za juu za uongozi.
Awali Wakili wa Serikali Kutoka Wizara ya katiba na Sheria na Mratibu wa Mafunzo Adv. Dorice Dario ameeleza malengo ya mafunzo hayo ni kuwawezesha Viongozi wa Serikali za Mitaa kuongeza ujuzi na maarifa yatakayo wasaidia kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayofikishwa mezani kwao.
Nao baadhi ya Watendaji wa Kata wameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwao, huku wakiahidi kuyatumia katika utekelezaji wa majukumu yao. Wakieleza kuwa uelewa mzuri wa sheria utawasaidia kusimamia haki na kuimarisha utulivu katika jamii.