Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WADAU WATAKIWA KUWASILISHA TAARIFA ZA HAKI ZA BINADAMU KWA WAKATI KUPITIA NALIS

Imewekwa: 27 Nov, 2026
WADAU WATAKIWA KUWASILISHA TAARIFA ZA HAKI ZA BINADAMU KWA WAKATI KUPITIA NALIS

Wadau wanaoandaa taarifa za utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali wametakiwa kutumia mafunzo waliyoyapata kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Huduma za Kisheria (National Legal Information System-NaLIS), kuhakikisha taarifa zinazoingizwa zinakuwa sahihi, kamili, zilizothibitishwa na zinawasilishwa kwa wakati.

Wito huo umetolewa leo Septemba 27, 2026, jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Kutoa Taarifa za Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Beatrice Mpembo aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadfamu, Bi. Nkasori Sarakikya wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya matumizi ya mfumo huo yaliyoratibiwa na Idara ya TEHAMA ya Wizara ya Katiba na Sheria. 

Bi. Mpembo amesema kuwa matarajio ya wizara ni kuona washiriki hao wanakwenda kuwa wasimamizi na waratibu wa matumizi ya mfumo wa NaLIS katika taasisi zao, kwa kushirikiana na watendaji wengine kwenye utekelezaji na uwasilishaji wa taarifa zinazohitajika.

Pia, Bi. Mpembo amebainisha kuwa washiriki hao wanapaswa kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Haki za Binadamu yanayotolewa kupitia Mikataba ya Kimataifa, Mfumo wa Mapitio ya Haki za Binadamu (UPR), pamoja na mifumo mingine ya kikanda na kitaifa kwa kushirikiana na vitengo na mamlaka husika.

Aidha, amewahimiza washiriki wote kutoa mrejesho kuhusu changamoto zozote watakazokutana nazo ili kuwezesha maboresho endelevu ya mfumo wa NaLIS, sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wengine wanaohusika na ukusanyaji na uandaaji wa taarifa hizo ili kuwepo na mwendelezo.

Mafunzo haya ya siku mbili yameratibiwa na Idara ya TEHAMA ya Wizara ya Katiba na Sheria yakiwa na lengo la kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mapendekezo ya vyombo vya kikanda na kimataifa vya Haki za Binadamu kupitia upatikanaji wa taarifa katika mfumo wa NaLIS ambapo jumla ya washiriki 21 kutoka katika idara na taasisi mbalimbali za kiserikali wameshiriki.