TANZANIA IMEWEKA MSISITIZO KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA YA MAENDELEO 2050
Ujumbe wa Tanzania unashiriki katika Kikao cha 89 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachofanyika jijini Dakar, Senegal kuanzia tarehe 12 hadi 21 Oktoba 2026, ukiangazia hatua madhubuti zinazochukuliwa na nchi ya Tanzania katika kuimarisha Utawala Bora.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Utekelezaji na Ufuatiliaji Haki za Binadamu Bw. Richard Kilanga amesema kuwa Tanzania imeweka mikakati ya kujenga misingi imara ya amani, usalama, na utangamano kama nguzo kuu za kufikia malengo ya Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa. Aidha, amesisitiza dhamira ya nchi katika kuoanisha vipaumbele vyake na utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 pamoja na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063.
Katika sekta ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Tanzania inawasilisha hatua kubwa zilizopigwa katika kuimarisha nishati safi ya kupikia, huduma za maji, elimu, afya, na miundombinu ya kimkakati. Serikali inaangazia uwekezaji mkubwa unaofanyika kwenye sekta ya kilimo, teknolojia, na ubunifu, mambo ambayo ni nguzo kuu za kitaifa katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kuanzia ngazi ya jamii.
Mbali na maendeleo ya kiuchumi, nchi inajivunia hatua kubwa zilizopigwa katika kulinda haki za kiraia, kisiasa, na kijamii chini ya falsafa ya 4R ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tanzania inaeleza jinsi falsafa hii inavyoendeleza mazungumzo ya kitaifa na wadau, kukuza uhuru wa vyombo vya habari, na kuimarisha uhuru wa kujieleza, huku ikihakikisha ulinzi wa utu wa mtu, demokrasia, na haki za makundi maalum kama wazee na watoto.
Kutokana na uwepo wa amani na utulivu, diplomasia ya uchumi ya Tanzania imeendelea kushika kasi ambapo nchi imekuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa ukiwemo Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mkutano wa COP 12, na Jukwaa la Uwekezaji kati ya EU na Tanzania. Aidha, katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Tanzania inajiandaa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Soka ya Afrika (AFCON) mwakani, yatakayoandaliwa kwa pamoja na nchi za Kenya na Uganda.