Tatueni Kero za Kisheria Zinazowakabili Wananchi – Dkt. Kazungu

Na William Mabusi – WKS Makete
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu amewataka Wataalam wanaotekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) kutatua kero za kisheria wanazokabiliana nazo wananchi na zile watakazoshindwa kutatua kuziacha zimeandaliwa nyaraka kwenda ngazi za juu kwa ajili ya kutatuliwa.
Dkt. Kazungu ameyasema hayo Mei 27, 2024 alipotembelea Timu inayotekeleza Kampeni ya Mama Samia katika Halmashauri ya Makete ambayo ilikuwa ikifanya mkutano na wananchi wa Kijiji cha Mago Kata ya Lupalilo.
”Tatueni changamoto za kisheria wanazokabiliana nazo wananchi hawa na kero zitakazowashinda kutokana na muda hakikisheni mnawaandalia nyaraka za kisheria ili waende ngazi zingine,” alisema.
Dkt. Kazungu aliwashukuru wananchi waliojitokeza kwenye kampeni hiyo na kutumia wasaa huo kuwazawadia pesa akina mama waliofika kwenye mkutano wakiwa na watoto wadogo.
Kabla ya kuanza kutekeleza kampeni Wilayani humo timu hiyo iliripoti ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kuongea na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Makete Bw. William Makufwe ambaye amewataka watekelezaji wa kampeni hiyo kutumia lugha inayoeleweka, "tumieni lugha nyepesi wakati mnatekeleza kampeni hiyo muhimu ya kutoa uelewa wa sheria ili Wananchi wawaelewe, lakini pia niwaombe kuangalia uwezekano wa kubadili ratiba yenu kwa kuongeza idadi ya vijiji kwa kuzingatia kwamba wananchi wetu ni wachache na baadhi ya vijiji viko karibu karibu."
Akifafanua juu ya fidia ya maeneo ya miradi, Bw. Advent Tweve, Afisa Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Makete amesema pale ambapo mradi umeombwa au kuibuliwa na kijiji ni wajibu wa kijiji kutoa eneo la mradi bure isipokuwa pale ambapo Serikali imeleta mradi na kupelekea uhitaji wa eneo, Serikali huwajibika kutoa fidia.
“Mnapoibua Miradi nakuhitaji eneo la mwanakijiji mwenzenu hakikisheni mnamwelewesha umuhimu wa mradi huo ili atoe eneo bure kwa hiari yake, tena mhakikishe mmeandikishana ili kuepuka migogoro hapo baadaye.” Alisema Bw. Tweve.