Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tufanye Kazi kwa Uadilifu na Ushirikiano - Mhe Chana

Imewekwa: 07 Nov, 2023
Tufanye Kazi kwa Uadilifu na Ushirikiano - Mhe Chana

Na George Mwakyembe – WKS Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka watumishi pamoja na Menejimenti ya Wizara yake kufanya kazi kwa kujituma, uadilifu na kwa ushirikiano ili kutimiza malengo ya Wizara katika kuwahudumia watanzania.

Waziri Chana ameyasema hayo tarehe 06/11/2023 Mtumba Jijini Dodoma yalipo Makao Makuu ya Wizara hiyo alipokutana na wafanyakazi na Menejimenti ya Wizara na kufanya nao Kikao Kazi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Akiongea kwenye kikao hicho Mhe. Chana alisema “dhamana tuliyopewa ya kuwahudumia wananchi ni kubwa na lazima tufanye kazi kwa bidii lakini pia kwa kujituma huku tukizingatia uadilifu na uaminifu.”

Aidha, Mhe. Balozi Chana ameongeza kuwa “Wizara ya Katiba na Sheria ni moja kati Wizara kongwe na muhimu sana hasa katika kusimamia sheria za nchi, na tayari tunaendelea na mchakato wa kutafsiri sheria zote za nchi na kuhakikisha sheria zote zinaandikwa kwa lugha ya Kiswahili.”

Naye Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amewataka watumishi kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa kujituma. Akiongea kwenye kikao hicho Mhe. Gekul amefafanua kuwa “Wizara ya Katiba na Sheria ina kazi nyingi za kuwahudumia wananchi ambazo zote ni za kutatua matatizo yao hivyo lazima tuwe wabunifu na wavumilivu na wenye lugha nzuri.”

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amefafanua kuwa mbali ya kuwa ikama ya watumishi ni 205 lakini tayari Wizara imendelea kupokea watumishi ambao wamekuwa wakihamia kutoka sehemu mbalimbali na kuongeza nguvu katika utendaji. Bi. Makondo ameongeza kuwa “sisi kama watumishi tumeakuwa tukiishi kama familia na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ikiwemo kuwa na mfuko wa kusaidiana pale mtumishi anapopata tatizo.”

Pia Bi. Makondo amemshukuru Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kushirki kwenye kikao cha pamoja na watumishi na kuahidi ushirikiano na mshikamano katika utendaji kazi.