Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tulistahili elimu hii: Wakazi wa Salawe

Imewekwa: 19 Jun, 2023
Tulistahili elimu hii: Wakazi wa Salawe

Na William Mabusi – WKS Shinyanga

Wananchi wa Kata ya Salawe na Solwa wamesema walistahili kupata elimu ya sheria na kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria kutokana na kuishi bila kujua sheria inasemaje kwenye maeneo mengi na kutokujua wapi wapeleke mashauri yao hasa ya ardhi baada ya kutofautiana na maamuzi ya mamlaka za chini na kutokujua namna ya kushughulikia kero za wasimamizi wa mirathi.

Mikutano katika Kata hizo mbili imefanyika kwa nyakati tofauti tarehe 16 Juni, 2023 ikiwa ni utekelezaji wa  Kampeni ya Msaada wa Sheria (MSLAC) katika Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga.

Bwana Heleman Mathias Sanane wa kijiji cha Mwanga Songambele kutoka Kata ya Salawe ameishukuru elimu ya sheria inayotolewa kwenye Kampeni hiyo kwa kusema "wananchi wengi tumevaa miwani ya mbao yaani mtu alikuwa anakabidhiwa usimamizi wa  mirathi halafu anasema ng`ombe wote wa marehemu  lete hapa, mashamba yote ya marehemu yako chini yangu. Yaani watu tumepoteza haki zetu kwa kutokujua sheria na ukijifanya kuhoji unatishiwa na kutakiwa kukaa kimya.”

Naye ndugu Bisanana Batemi mkazi wa Solwa amesema “elimu inayotolewa ni uhitaji wa kila mtu na hasa wananchi wa vijijini ambao hatuna uelewa mkubwa wa sheria na mabadiliko yake, sasa tumeelewa faida za kumiliki ardhi kisheria na jinsi ya kugawana mali za ndoa.”  akalinganisha utamu wa elimu ya sheria iliyotolewa kama asali.

Akitoa mada katika mikutano hiyo Wakili wa kujitegemea Bw. Chrisatus Chengula kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika ameyataja mambo ya kuzingatia wakati ardhi inahamishwa kutoka kwa mmiliki mmoja kwenda kwa mwingine kuwa ni pamoja na mauziano hayo kuwekwa kwenye maandishi na yasainiwe mbele ya mamlaka ya Serikali ya eneo husika endapo hakuna Mwanasheria eneo hilo.

Kuhusu ardhi anayomilikishwa mtu kama zawadi au urithi, mmiliki ahakikishe anaomba hati ya maandishi ya zawadi ambayo itatumika kama kumbukumbu na itatumika wakati wa kuomba kuthibitishwa umiliki wa eneo husika kisheria.

Wakili huyo alisema msimamizi wa mirathi ambaye anaenda kinyume na taratibu za kisheria, familia ina wajibu kisheria kwenda mahakamani na kuomba kutengua usimamizi wake. Kwa kuwa mashauri ya mirathi hayana ukomo wananchi ambao hawajafungua mirathi waliombwa kufungua mirathi ili kuepusha migogoro mingi inayotokea katika familia baada ya mzazi au wazazi wote kufariki dunia.

Aidha, ilielezwa kwamba Mamlaka ya chini kabisa katika kushughulikia mgogoro wa ardhi ni Mabaraza ya Kata. Kabla ya mwaka 2021 Mabaraza hayo yalikuwa na mamlaka kimahakama ya kutoa uamuzi lakini kuanzia 2021 sheria hiyo ilibadilishwa na sasa Mabaraza hayo yanatakiwa kusuluhisha tu mgogoro wa ardhi. Endapo mgogoro huo ukishindikana Baraza huandika hati ya kushindwa kusuluhisha mgogoro husika na hati hiyo kupelekwa Baraza la Nyumba na Ardhi la Wilaya. Endapo mlalamikaji hataridhika na uamuzi wa Baraza la Wilaya atakata rufaa kwenda Mahakama Kuu, Kama bado hataridhika ataenda Mahakama ya Rufaa.