Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tushirikiane Kutekeleza MSLAC Singida: Dkt. Kazungu

Imewekwa: 04 Jan, 2024
Tushirikiane  Kutekeleza MSLAC Singida: Dkt. Kazungu

Na William Mabusi – WKS Singida

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu ametoa wito kwa Mkoa wa Singida kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wote wa utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign - MSLAC) inayotegemewa kufanyika mkoani humo kuanzia tarehe 10 hadi 19 Januari, 2024.

Dkt. Kazungu ametoa wito huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Sekretarieti ya Mkoa wa Singida tarehe 04 Januari, 2024 kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa, akiwa ameongozana na sehemu ya Menejimenti ya Wizara. Kikao kazi hicho kililenga kufanya tathmini ya awali ya maandalizi ya MSLAC ambayo itatekelezwa kwenye Halmashauri zote saba mkoani humo.

“Kikubwa ambacho Wizara inaomba kutoka kwenu ni ushirikiano mkubwa ili kufanikisha Kampeni hii. Kote ambako tumetekeleza kampeni hii tumepata ushirikiano wa kutosha na sasa ni zamu yenu.” Alisema na kuongeza kuwa wananchi wahamasishwe kufika kwa wingi siku ya uzinduzi lakini pia kwenye maeneo ambayo mikutano ya kutoa elimu na huduma ya msaada wa kisheria itakuwa inafanyika.

Akitoa maelezo ya maandalizi yaliyofanyika kwa upande wa mkoa, Msajili Msaidizi wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria mkoani humo Bi. Shukrani Mbago amesema Halmashauri zote saba zimetaarifiwa kuhusu kufanyika kwa kampeni hiyo, Kata zote ambazo zitapitiwa na kampeni zimeshaandaliwa, wamekaa na Watoa huduma za kisheria, mkoa umeunda Kamati ya maandalizi ya uzinduzi wa Kampeni. Aidha, mialiko mbalimbali imetolewa kwa Taasisi na Wadau muhimu wanaotakiwa kushiriki Kampeni pamoja na maandalizi ya bajeti ya kutekeleza Kampeni mkoani humo.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Bw. Stanslaus Beatus Choaji amesema Mkoa wake utafanya yote yanayohitajika kufanya kampeni hiyo itekelezwe kama ilivyopangwa. Aidha, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuja na mpango huu wa kutetea haki kwa wananchi wanyonge.