"Tuwasaidie Wananchi Kutatua Migororo Kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia" – Sagini

Hyasinta Kissima - WKS Njombe
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amewataka Wataalamu watakaoshiriki katika zoezi la utoaji msaada wa kisheria katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia "Mama Samia Legal Aid Campaign" kuhakikisha wanatoa elimu kikamilifu ili kutatua migogoro na kero za Wananchi.
Mhe. Sagini ameyasema hayo Mei 25, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa Wataalamu watakaoshiriki katika zoezi la kutoa msaada wa Kisheria kwa muda wa siku kumi katika Halmashauri sita za Mkoa wa Njombe.
"Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameanzisha Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ili kuhakikisha kuwa kila Mwananchi ambaye hana uwezo wa kuwafikia Mawakili na Wanasheria kunufaika na huduma hii. Kampeni hii imekua na manufaa makubwa sana kwa Wananchi. Ninaamini ninyi mlioaminiwa kufanya kazi hii mtathamini uzito huu ambao Mhe. Rais ameuweka kupitia kampeni hii." Alisema Mhe. Sagini.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Sagini ameelekeza ni vyema Wizara ya Katiba na Sheria ikaona umuhimu wa kufanya tafiti mbalimbali ili kuona madhara yatokanayo na watu kushindwa kufahamu haki zao Kisheria ambapo wakati mwingine malalamiko hayo huenda yakasababishwa na Watumishi wa Umma wasiotimiza wajibu wao ipasavyo.
Tangu kuzinduliwa kwa Kampeni hiyo Kitaifa, Njombe ni Mkoa wa saba utakaoenda kunufaika na msaada huo wa Kisheria, na jumla ya Wataalamu 86 wamepatiwa mafunzo hayo watakaotoa msaada huo katika Halmashauri sita za Mkoa wa Njombe.