Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Ujenzi wa Mahakama za Wilaya na za Mwanzo Unaendelea – Sagini

Imewekwa: 16 Apr, 2024
Ujenzi wa Mahakama za Wilaya na za Mwanzo Unaendelea – Sagini

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama kwa awamu kote nchini.

Mhe. Sagini ameyasema hayo wakati akijibu swali kutoka kwa Mbunge wa Kalambo Mhe. Josephat Sinkamba Kandege Bungeni tarehe 16 Aprili, 2024 Jijini Dodoma.

Katika swali lake la msingi lililoulizwa na Mhe. Rashid Shangazi kwa niaba yake, Mhe. Kandege alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kujenga na kukarabati Mahakama za Mwanzo Wilayani Kalambo.

Katika kuweka msukumo wa ujenzi wa majengo ya Mahakama kote nchini Mhe. Sagini amesema ”Serikali ina Mpango wa ukarabati na ujenzi wa Mahakama kwa awamu. Kupitia Mpango huo katika mwaka wa fedha 2019/20 imeshajengwa Mahakama ya Mwanzo ya Msanzi katika jimbo la Kalambo. Pia katika mwaka wa fedha 2023/24 Mahakama ya Wilaya pamoja na Mahakama ya Mwanzo ya Kasanga zinajengwa.”

Akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mhe. Shangazi aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani mahususi wa kukarabati Mahakama ya Mwanzo au kujenga Mahakama mpya kwenye Tarafa ya Mlalo, Mhe. Sagini amesema katika Mwaka wa fedha 2024/25 jumla ya Mahakama za Mwanzo 72 ziko kwenye mpango wa kukarabatiwa hivyo atawasiliana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama kujua Mahakama hiyo imewekwa awamu ipi.