Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Vijana Jitumeni Katika Masomo Fursa Kwenye Kada ya Sheria ni Nyingi - Chana

Imewekwa: 12 Sep, 2023
Vijana Jitumeni Katika Masomo Fursa Kwenye Kada ya Sheria ni Nyingi - Chana

Na Lusajo Mwakabuku – WKS Dar es Salaam

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (MB) amewataka wanafunzi wanaoendelea na masomo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria Kwa Vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) kujituma zaidi katika kuhakikisha wanafaulu vizuri ili kuweza kukidhi fursa mbalimbali zilizopo nchini ambazo zinahitati kada ya uanasheria.

Waziri Chana amesema hayo wakati wa ziara yake ya kwanza chuoni hapo tangu kuapishwa kwake kuwa Waziri wa Katiba na Sheria tarehe 12/09/2023  ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wanafunzi hao kuishi katika taaluma yao kivitendo kwa kuutumia utaalamu wao wakianzia ngazi ya familia.

“Wewe kama mwanasheria unatakiwa tokea eneo unaloishi wakutambue kwamba wewe ni msomi uliyebobea katika masuala ya sheria, watakutambua kwa namna utakavyoweza kutekeleza majukumu madogo madogo ya kisheria katika maeneo yako, nafasi za ajira ni nyingi kuanzia kwenye sekta za uma mpaka makampuni binafsi” Alisema Mhe. Chana.

Akiongea na watumishi pamoja na uongozi wa  Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria Kwa Vitendo Tanzania, Waziri wa Katiba na Sheria amewataka watumishi kutambua kuwa wamebeba dhamana kubwa kwa Taifa na kwamba yeye kipaumbele chake kiko kwenye maslahi ya watumishi likiwa ni suala muhimu katika kuhakikisha matokeo mazuri ya kazi.

“Ili ng’ombe uweze kumkamua vizuri na upate maziwa mengi ni lazima uhakikishe anapata majani na maji ya kutosha ili mwili uweze kuwa na afya, hivyo na mimi nitahakikisha napambania maslahi yenu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mnatengewa bajeti yenu wenyewe ili muweze kumudu miundombinu ya utekelezaji wa majukumu yenu,” aliongeza Waziri Chana.

Awali akimkaribisha Waziri, Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo alisema ni wakati muafaka sasa kwa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria Kwa Vitendo Tanzania (Law School) kutengeneza kanzidata ya wanaomaliza katika chuo hicho ili waungane na kampeni inayoendelea nchini kote ya Mama Samia Legal Aid katika kuhakikisha haki inawafikia hata wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili.

Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. Sist J. Mramba alisema katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za kisheria, Taasisi imeanzisha programu maalum kwa wasaidizi wa kisheria kwa ngazi ya cheti na diploma lengo likiwa ni kutoa wataalam watakaoweza kuwasaidia wananchi wa hali ya chini wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili.