Vijana Watoa Msaada Wa Kisheria Wampongeza KM Maswi
Ikiwa ni miezi minne tangu vijana wapatao 12 wenye taaluma ya Sheria walipojiunga na Wizara ya Katiba na Sheria na kushirikiana na Wataalamu wa Wizara katika mafunzo kwa vitendo vijana hao wameonesha kuguswa na kumkabidhi zawadi ya pongezi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Eliakim Maswi kwa utendaji kazi wake na moyo wa kuwajali.
Wakizungumza mara baada ya kumtembelea Katibu Mkuu ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma leo tarehe 10 Januari, 2025 mwakilishi wa vijana hao Prisila Kayuli amesema kuwa kwa kipindi chote wameshiriki na kupata ushirikiano ipasavyo katika shughuli mbalimbali za Wizara bila kuwa na ubaguzi jambo ambalo limewafanya wao kuwasilisha pongezi hizo ili kumtia moyo na kutambua mchango wake kwa kulitambua kundi hilo la vijana katika kuhakikisha wanapikwa ipasavyo katika sekta ya Sheria ili baadaye wawe Watendaji bora na wenye maadili.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Bw. Eliakim Maswi amewataka vijana hao kuendelea kujifunza kwa bidii pindi wanapopata nafasi kama hizo, kumtanguliza Mungu na pia kuhakikisha wanakuwa na ndoto za kufika mbali.
Maswi ameongezea kuwa, furaha yake ni kuona Wataalamu wa Wizara na wale wanaofika katika Wizara kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali wanakuwa ni wachapakazi, wabunifu ili sekta ya Sheria iwe na Wanasheria wenye weledi katika kazi na wanaoweza kusimama bila woga na bila kubabaishwa katika kutetea maslahi ya Taifa la Tanzania.